NA MARCO KANANI, GEITA
MKAZI wa Isabageni wilayani Sengerema, Zakharia Tabaro, amedaiwa kuuawa kwa kupigwa na walinzi wa mgodi wa dhahabu wa Geita kisha kuwekewa jiwe kubwa kifuani.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi, ambapo inadaiwa Tabaro (35) aliingia mgodini humo kwa muda usiojulikana kwa lengo la kuchukua mawe yanayodaiwa kuwa na dhahabu maarufu kama magwangala.
Akizungumza kwa masikitiko, mmoja wa ndugu wa marehemu, Mengi Paulo alisema Tabaro aliondoka Mugusu mjini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita bila kufahamika mahali alipokwenda.
Juhudi za kumtafuta zilifanyika bila mafanikio hadi juzi alfajiri, walipopata taarifa kwa baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo kwamba kuna mtu amekufa ndani ya mgodi.
Alisema baada ya taarifa hizo, saa tatu asubuhi, waliingia mgodini humo na kuikuta maiti ya ndugu yao ikiwa na jeraha kubwa usoni linalosadikika kupigwa kwa mawe, huku kifuani akiwa amewekewa jiwe zito.
"Ndugu mwandishi imekuwa ni kawaida yao walinzi wa mgodi kuua watu wanaowakamata ndani ya eneo la mgodi, ni vyema wawakamate na kuwapeleka polisi na si kuwaua," alisema Paulo.
Ofisa Habari wa Mgodi wa Geita (GGM), Tenga Birri Tenga, alipoulizwa alikanusha mauaji hayo kufanywa na walinzi wa mgodi na kudai kuwa, huenda alipigwa na wachimbaji wake kisha kumtupa eneo la mgodi.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Pundensiana Protas, hakupatikana kutokana na kuwa kwenye mkutano kwa mujibu wa mlinzi wake, ambaye muda wote alikuwa akishikilia simu yake ya kiganjani.
Mwili wa marehemu ulichukulia na polisi kutoka mgodini humo na kupelekwa Hospitali ya Wilaya kwa uchunguzi zaidi.
Kumekuwa na uhusiano usioridhisha baina ya mgodi na wananchi wanaozunguka maeneo ya mgodi, ambapo Ofisa Uhusiano wa GGM, Joseph Mangirima, amekuwa kwenye jitihada za kuimarisha uhusiano kwa kukutana na wananchi na kufanya vikao.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru