Tuesday, 8 October 2013

Mzee Mwinyi afichua siri ya uongozi wake


Na Hamis Shimye
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuthubutu kuwapeleka mahakamani viongozi wa serikali yake wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali, ikiwemo matumuzi mabaya ya madaraka.
Hata hivyo, amesema anashangazwa na ukimya wa vyombo vya sheria katika kuchukua uamuzi dhidi ya watu hao.
Aidha, amesema changamoto zinazojitokeza katika Muungano hivi sasa, zinapaswa kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi.
Mzee Mwinyi alisema hayo jana, alipohojiwa na gazeti hili kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea nchini, ambapo alisema Rais Kikwete amefanya kazi kubwa, ambayo awali ilikuwa ngumu kutekelezeka.
Alisema huko nyuma ofisa wa serikali akipelekwa mahakamani ni kashfa kubwa na ikitokea, huondolewa kazini bila kufanywa chochote.
“Rais Kikwete anastahili pongezi. Uadilifu ni jambo muhimu, lakini awali lilikuwa gumu, hasa pale anapotokea ofisa wa serikali kafanya ubadhirifu, utafuatwa Ikulu na kuambiwa mheshimiwa kuna hili na kuelezwa, lakini ni aibu kwa serikali ukichukua uamuzi,” alisema.
Alisema katika utawala wa awamu ya nne, mambo hayo hakuna na ameshuhudia viongozi wengi wakipanda kizimbani kwa tuhuma zinazowakabili.
Hata hivyo, alisema anashangazwa na vyombo vya sheria kushindwa kuchukua uamuzi wa haraka, hasa baada ya Rais Kikwete kuwa mstari wa mbele katika mapambano hayo.
“Haiwezekani mtu anachukua miaka sita hukumu haijatolewa, hii inarudisha nyuma ari ya mapambano na hayataweza kwisha, hasa wakati ambapo Rais Kikwete hataki kupelekewa majina Ikulu ya watu wasio waadilifu na badala yake watu hao wapelekwe mahakamani,” alisema.
Alisema kuchukuliwa hatua kwa watu hao, kutasaidia kumaliza tatizo la watumishi kutokuwa waadilifu, hasa kwenye fedha za umma.
MUUNGANO HAUPASWI KUVUNJWA
Alisema mambo mengi yanasemwa kuhusu Muungano, ambapo baadhi wamekuwa wakishauri uvunjwe, wengine wakitaka muundo wa serikali tatu na wengine wakitaka kuendelea kwa utaratibu wa serikali mbili.
“Binafsi napenda Muungano udumu kwa kuwa ni mapinduzi na umoja katika kusaka maendeleo. Nakumbuka kipindi cha nyuma kabla ya Muungano, Mwalimu Julius Nyerere alituambia mambo mengi, ikiwa ni pamoja na umuhimu wa Muungano,” alisema.
Alisema Mwalimu Nyerere alikuwa anatamani Muungano kwa kuwa aliamini ni umoja na ni nguzo muhimu kwa uchumi imara. Nchi nyingi zimeshindwa kufanya hivyo, wakati Tanzania na Zanzibar zimefikisha miaka 50.
Kwa mujibu wa Mzee Mwinyi, kabla ya kuungana na Zanzibar, Mwalimu akiambatana na aliyekuwa Rais wa Uganda wakati huo, Milton Obote alikwenda Kenya, na kumuomba Rais Jomo Kenyatta kutaka kuungana.
“Katika watu 100 lazima mtatofautina kwa kuwa kufanya hivyo si kosa, bali kinachohitajika ni ustahimilivu na kuvumiliana. Uitishwe mjadala watu wazungumze ili mambo yamalizwe na Muungano uendelee.
Alisema nchi za nje wanaungana katika mifumo tofauti kwa lengo la kuimarisha umoja na hakuna tatizo.
G55 LAMPA MTIHANI
Mzee Mwinyi ambaye alikuwa madarakani kuanzia mwaka 1984 hadi 1995, anasema miongoni mwa mambo yaliyompa wakati mgumu na kumwudhi ni muungano wa kundi la wabunge lililojulikana kama G55.
“Ulikuwa ni mtihani mkubwa sana kwangu, ila nashukuru tuliumaliza vyema pamoja na kumuomba Mwalimu Nyerere katika suala hilo ambalo ugumu wake ulitokana na watu waliokuwa katika kundi hilo kuwa wabunge... hawa hawakuwa wananchi wa kawaida,” alisema.
Alisema ilikuwa vigumu kuchukua hatua za moja kwa moja dhidi ya kundi hilo kwa kuwa liliundwa na wabunge, hivyo ulihitajika umakini mkubwa wakati wa kushughulikia tatizo hilo.
G55 ni kundi la wabunge wa CCM waliokuwa wakiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Lupa, Njelu Kasaka, ambao walitaka kupeleka hoja binafsi bungeni wakitaka kuanzishwa kwa serikali ya Tanganyika na kushauri Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uvunjwe.
ZIMBABWE, INDIA
ZILITUKOPESHA FEDHA
Mzee Mwinyi alisema wakati anaingia madarakani aliikuta nchi ikiwa katika hali ngumu kiuchumi, kwa kuwa HAZINA (Wizara ya Fedha) haikuwa na fedha, serikali ikikabiliwa na matatizo katika ulipaji mishahara wa wafanyakazi.
“Wakati huo ndio tulikuwa tumetoka katika vita vya Kagera na ilikuwa lazima tupambane na kuikomboa nchi. Nilipoingia nikakumbana na mambo hayo, ikiwemo vikwazo vilivyotokana na sera zetu za kiuchumi,” alisema.
Alisema nchi nyingi zilikataa kuisaidia Tanzania kutokana na sera zake, na kwamba ilibidi kumtumia Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kwenda kwa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kukopa fedha pamoja na Waziri Mkuu mstaafu Dk. Salim Ahmed Salim kwenda India.
“Naweza kusema hizi zilikuwa kama ‘kishika uchumba’, kwani nilipata dola milioni 100, kwa Mzee Mugabe pamoja na Dk. Salim kwenda India kuomba dola milioni 100 zingine, ambazo zote tulilipa na hata kuisaidia nchi kufanya mambo mbalimbali,” alisema.
Alisema fedha hizo zilisaidia mambo mengi na hata kuiwezesha taifa kufanya mambo mengi, ikiwemo kuimarisha shughuli za kiuchumi na maendeleo, huku wananchi kufanya mambo yao bila matatizo yeyote.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru