Tuesday, 8 October 2013

Vijana na tatizo la ajira


MOHAMMED ISSA
WIZARA ya Kazi na Ajira, imesema tatizo la ajira kwa vijana ni kubwa na serikali inapaswa kuweka miundombinu mizuri.
Imesema takwimu zinaonyesha kuwa, kila mwaka watu milioni moja huingia kwenye soko la ajira, ambapo kati ya hao 40,000 ndio wanaoajiriwa serikalini kila mwaka.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) mjini Dar es Salaam, jana, Mchumi Mwandamizi wa Wizara hiyo, Geofrey Mashafi alisema ili kumaliza tatizo hilo, lazima Sera ya Ajira ya Mwaka 2008 isimamiwe ipasavyo.
Alisema sera hiyo itaziwezesha sekta binafsi kutoa ajira kwa wingi, hasa vijana wengi kuajiriwa na sekta hiyo na hivyo kumaliza tatizo hilo.
Mashafi alisema taifa linakabiliwa na changamoto kubwa ya ajira kwa vijana, hivyo juhudi mbalimbali zichukuliwa kumaliza tatizo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara hiyo, Ridhiwani Wema alisema sekta za viwanda na kampuni za ulinzi binafsi zinaongoza kwa malalamiko ya wafanyakazi.
Alisema wafanyakazi wa sekta hizo, wanazilalamikia kutokana na kupata maslahi madogo wanayolipwa na waajiri wao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru