Wednesday 9 October 2013

Wapinzani wababaishaji-ZANU-PF




Na Hamis Shimye
WATANZANIA wametakiwa kuwa makini na vyama vya upinzani, kwani vingi havina dira wala mwelekeo wa kuwasaidia wananchi, kwani uanzishwaji wake umejaa ubabaishaji.
Mbali na hilo, wana-CCM wameaswa kuhakikisha CCM inaendelea kubaki madarakani kwa kuwa ni chama chenye mtazamo wa kimaendeleo.
Katibu Mkuu wa Chama cha ZANU-PF cha Zimbabwe, Didymus Mutasa, aliyasema hayo jana mjini Dar es Salaam, katika kikao cha Makatibu Wakuu wa Vyama vya Ukombozi Kusini mwa Afrika.
Mutasa alisema vyama vya upinzani si vyama makini, hivyo haviwezi kuwasaidia wananchi kutokana na uanzishwaji wake kuwa wa ubabaishaji na havina mtazamo wa kimaendeleo.
“Afrika hakuna vyama vya upinzani na Watanzania wasikubali kabisa, kwa kuwa vyama hivyo havina mwelekeo kutokana na kutokuwa na mizizi katika uanzishwaji wake tofauti na vyama tawala,” alisema.
Mutasa alisema vyama vingi vya upinzani vimeletwa na nchi za Magharibi ili kunyonya na kupora rasilimali zilizo ndani ya Afrika, hivyo wasikubali kuvipa nafasi.
Aliwaonya Watanzania kutokubali kamwe kuona CCM inaondoka madarakani na kuja chama kingine, kwa kuwa vyama hivyo havitakuwa na uwezo wa kuwaletea maendeleo.
Kwa mujibu wa Mutasa, siri kubwa ya ushindi wa ZANU-PF katika uchaguzi mkuu wa Zimbabwe, uliofanyika hivi karibuni na Rais Robert Mugabe kuibuka mshindi ulitokana na Wazimbabwe kutokubali kuwapa wapinzani nchi kusimamia sera ya uwekezaji.
“Tuna hakika tunapendwa na Wazimbabwe, hasa kutokana na serikali kuwa wazi na kuhakikisha inasimamia rasilimali za nchi na hata kusikiliza vilio vyao. Hivyo, ushindi wetu ni sauti ya Wazimbabwe,” alisisitiza.
Alisema hata kelele kwamba Rais Mugabe ni mzee na mwenye umri mkubwa, hazikufanikiwa, kwani wapinzani walisahau hata Malkia Elizabeth II wa Uingereza ni mzee kuliko hata Zimbabwe yenyewe.
“Malkia ni mzee kuliko Zimbabwe yenyewe na bado ni Malkia wa Uingereza. Hivyo Mugabe ni Rais wetu na bado Wazimbabwe wanampenda,” alisema.
Mapema, akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa unavikutanisha vyama vilivyoleta ukombozi na watautumia kujadili masuala mbalimbali muhimu.
Alisema kila chama kitakuwa na ajenda yake katika mkutano huo, ambapo ajenda kuu itakuwa vijana, hasa kutokana na changamoto kadhaa zinazowakabili.
Mkutano huo wa siku moja, ulimalizika jana kwa viongozi hao kufikia maazimio mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuamsha serikali zao kuboresha maisha ya wananchi katika nchi hizo.
Mbali ya CCM na ZANU-PF, vyama vingine ambavyo vilishiriki mkutano huo ni MPLA ya Angola, Frelimo ya Msumbiji, ANC ya Afrika Kusini, SWAPO ya Namibia na Chama rafiki cha Kikomunisti cha China (CPC).


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru