Tuesday 22 October 2013

Nyaisanga aagwa Dar, James Kombe afariki


JUMANNE GUDE NA PAUL NKURUS
WAKATI Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal, akiwaongoza mamia ya wakazi wa jijini Dar es Salaam na wanahabari kuuaga mwili wa mtangazaji mkongwe Julius Nyaisanga ‘Uncle J’, Watanzania jana walipata pigo lingine kufuatia kifo cha aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, James Kombe.
Kamanda Kombe, alifariki jana katika Hospitali ya Ocean Road alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mwili wa marehemu Nyaisanga uliwasili katika viwanjani vya Leaders saa 11.30 asubuhi, huku mamia ya watu walimiminika kuuaga mwili wa mtangazaji huyo nguli nchini.
Baadhi ya waandishi wakongwe waliofika kumuaga mwenzao ambaye waliwahi kufanya naye kazi ni pamoja na Michael Enock Ngombale, ambaye ndiye aliyempa marehemu jina la Uncle J, Abubakar Liongo, Abdallah Majura, Masoud Masoud, Betty Mkwasa na Mikidadi Mahamud.
Nyaisanga aliyewahi kufanya kazi Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), hivi sasa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kampuni ya IPP Media, mpaka mauti yanamkuta alikuwa Mkurugenzi wa Abood Media,
Akitoa salamu za pole kwa niaba ya serikali na Watanzania, Makamu wa Rais Dk. Bilal, alisema Nyaisanga alitoa mchango mkubwa kwa taifa na alikuwa mahiri katika kazi yake ya utangazaji.
Alisema marehemu alikuwa maarufu kutokana na sauti yake, ubunifu wa namna ya kutangaza vipindi na taarifa za habari, hali iliyomfanya awe na mashabiki wengi ambao walipenda kila kazi aliyokuwa akiifanya ihusuyo habari.
Alisema taifa limempoteza mwanahabari huyo ambaye daima alikuwa karibu na watu.
Mwili wa marehemu ulisafirishwa jana kwenda Tarime, Mara kwa maziko.
Akizungumzia kifo cha Kamanda Kombe, Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Advera Senso, alisema utaratibu wa mazishi ya unaendelea na taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
Advera, alisema Kombe alizaliwa mwaka 1950 huko Mwika mkoani Kilimanjaro na alijiunga na Jeshi la Polisi Machi 15, mwaka 1970, baada ya kuhitimu elimu ya sekondari mwaka 1969 nchini Uganda, ambapo alipandishwa vyeo na kupewa madaraka mbalimbali.
Baadhi ya vyeo alivyopitia na miaka ya katika mabano ni Sagenti wa Polisi (1973) Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (1977), Mkaguzi wa Polisi (1984), Mrakibu Msaidizi (1986), Mrakibu wa Polisi (1991), Mrakibu Mwandamizi (1995), Kamishna Msaidizi wa Polisi (1998) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (2002) hadi alipostaafu mwaka 2010.
Baadhi ya nafasi alizowahi kuzitumikia katika Jeshi la Polisi ni pamoja na Ukuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) katika wilaya za Dodoma, Tarime, Serengeti na Arusha.
Pia alishika nafasi ya Mkuu wa Polisi Mkoa (RPC) mkoani Lindi, Arusha na Kigoma kabla ya kuwa Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza ghasia Tanzania.
Mpaka anastaafu, marehemu Kombe Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Tanzania.
Mhariri na Wafanyakazi wa Uhuru Publications Ltd, wanatoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki wote walioguswa na misiba hii.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru