Na Hamis Shimye
SERIKALI imesema ipo katika mchakato wa kuanzisha mpango wa maendeleo ya elimu ya juu ili kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ya juu nchini.
Pia, imewataka wazazi na walezi nchini, kuwatilia mkazo watoto wao kusoma masomo ya sayansi ili kusaidia harakati za serikali katika kuboresha kiwango cha elimu.
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, aliyasema hayo jana alipokuwa akizindua mradi wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu (STHEP), katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Alisema mradi huo ni sehemu ya mikakati ya kuboresha sayansi nchini.
Dk. Bilal, alisema serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB), imetekeleza mradi huo kwa dhumuni la kuongeza idadi ya wahitimu na kuwapa uwezo walimu katika ufundishaji wa masomo ya sayansi na teknolojia.
“Sayansi na teknolojia ni muhimu, wazazi, na walezi wanapaswa kuwapa moyo watoto wao wa kusoma masomo haya kwa kuwa ni muhimu katika ustawi wa maisha ya dunia ya sasa,” alisema.
Dk. Bilal, alisema utekelezaji wa mradi huo, ni moja ya vipaumbele ambavyo serikali imejiwekea katika kuhakikisha inatekeleza dira ya maendeleo ya mwaka 2025 kwa kujenga mazingira bora ya ufundishaji masomo ya sayansi.
Pia, alisema serikali imepanga kutekeleza sera mbalimbali ikiwemo ya kuhakikisha ina maliza tatizo la uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na hesabu.
Alisema mradi huo utakuwa chachu ya ongezeko la ukuaji wa masomo ya sayansi nchini yatakayosaidia kupatikana kwa walimu wengi wenye uwezo katika masomo hayo.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema utekelezaji wa mradi huo ni moja ya mipango ya wizara ya kuhakikisha ina maliza matatizo katika masomo ya sayansi hasa kwa kupata walimu.
Mradi wa STHEP umefadhiliwa na WB na umeegemea katika mambo mbalimbali, ikiwemo kuwasomesha walimu katika viwango vya shahada ya uzamili na uzamivu katika masomo ya sayansi na kujenga maabara, kununua vitendea kazi na ofisi.
STHEP umeshaanza kutekelezwa katika vyuo mbalimbali kikiwemo DUCE, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu Huria cha Dar es Salaam (UDSM).
000
Thursday, 24 October 2013
Mpango maendeleo elimu ya juu waja
00:36
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru