Thursday 31 October 2013


Tanzania yaruka ‘kimanga’ EAC
SERIKALI imesema masuala yanayojadiliwa na kuamuliwa nje ya utaratibu wa Jumuia ya Afrika Mashariki, haiyatambui kama uamuzi wa jumuia na utekelezaji wake utazihusu nchi za Kenya, Rwanda na Uganda pekee.
Pia, imewataka wananchi watambue kuwa, serikali ipo makini katika kufuatilia masuala yanayotokea katika jumuia hiyo.
 Katika kuonyesha umakini huo wa serikali, kwa sasa, imesema ipo katika majadiliano na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Burundi, kuona namna ya kuanzishwa kwa ushirikiano kama nchi za Rwanda, Kenya na Uganda zikiendeleza mkakati wa kuzitenga baadhi ya nchi wanachama.
Msimamo huo wa serikali ulitolewa juzi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, mjini hapa, alipomjibu Rukia Ahmed (Viti Maalum -CCM), aliyetaka kujua msimamo wa serikali juu ya mambo yanayohusu Jumuia ya Afrika Mashariki kujadiliwa na kutolewa uamuzi bila Tanzania kushirikishwa.
Rukia, alisema katika mkutano uliofanyika wakati wa ufunguzi wa Bandari ya Mombasa, masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na biashara, miundombinu na Shirikisho la Afrika Mashariki kwa kuzihusisha Rwanda, Kenya na Uganda, huku Tanzania na Burundi zikitengwa.
Katika maelezo yake, Sitta alisema tayari Tanzania imeomba ufafanuzi kwa kumtaka Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri anayetoka Uganda, kutoa taarifa ya kina kuhusu mikutano hiyo ya utatu inayoendeshwa sambamba na mikutano ya kawaida ya kalenda ya jumuia.
Aidha, Sitta akijibu maswali ya Hamad Rashid Mohamed (Wawi - CUF) na John Komba (Mbinga Magharibi - CCM) waliotaka kujua kwa nini Tanzania isijitenge na jumuia hiyo na kuunda jumuia yake mpya, alisema wameshaanza majadiliano na DRC na Burundi.
“Mara nyingi matatizo ya Afrika yanachangiwa na viongozi, tunajua kwa nini Rwanda inatununia, lakini wakati ukifika tutachukua hatua, maana tuko makini kulinda maslahi ya taifa letu,” alisema Sitta.
Alisema si kwamba Tanzania imekaa kimya wakati Rwanda, Kenya na Uganda zikianza mchakato wa kuanzisha mambo yao, bali kwa sasa, serikali ipo katika majadiliano na DRC na Burundi wa kutaka kuanzisha ushirikiano.
Akijibu swali la Anne Kilango-Malecela (Same Mashariki - CCM), aliyetaka serikali kutoshiriki tena katika uamuzi wowote mpya katika jumuia mpaka pale mtengamano utakapopatikana, Sitta alisema kazi hiyo tayari imeanza.
“Si kwamba tumekaa kimya kwa utoto huu unaoendelea kufanywa, hatuwezi kuvumilia mchezo huu wa kuigiza, tayari tumeshamwagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatiafa (Bernard Membe), kutoshiriki mkutano wa mawaziri hao watakaokutana kesho (jana) Kigali,” alisema.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru