Na Nathaniel Limu, Singida
DIWANI wa kata ya Iseke (CHADEMA), Emmanuel Jingu, amepandishwa kizimbani kujibu mashitaka ya kuvunja ofisi ya kijiji cha Nkhoiree na kuiba vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya sh. 200,000.
Jingu alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida na kusomewa mashitaka na Wakili Petrida Muta, mbele ya Hakimu Asha Mwitendwa.
Muta alidai mshitakiwa alitenda makosa hayo, Septemba 20, mwaka huu, saa 8.30 mchana, ambapo alivunja nyumba kwa lengo la kuiba mali.
Ilidaiwa mshitakiwa huyo, baada ya kuvunja mlango wa nyumba inayotumiwa na serikali ya kijiji cha Nkhoiree, aliiba vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh. 298,000.
Mshitakiwa huyo alidaiwa kuiba vocha, vitabu vya risiti, kitabu cha malipo, risiti za ushuru, hati za malipo, vitabu vya ushuru, risiti za zahanati na madumu matupu 100.
Jingu alikana mashitaka na alirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Masharti ya dhamana ni kuwa na mdhamini mmoja atakayetia saini bondi ya sh. 500,000. Kesi hiyo itatajwa Novemba 11, mwaka huu.
Tuesday, 29 October 2013
Diwani CHADEMA kortini kwa wizi
08:47
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru