Tuesday 8 October 2013

Iringa yaanza kufurika


Na Tumaini Msowoya, Iringa
MKUU wa Mkoa, Dk. Christine Ishengoma, amewaonya wafanyabiashara kutopandisha bei za bidhaa, ikiwemo vyakula pamoja na nyumba za kulala wageni wakati wa Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Mbali na maadhimisho hayo, mkoa utakuwa mwenyeji wa Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na Wiki ya Vijana, ambayo tayari imeshaanza.
Kutokana na sherehe hizo za kitaifa, mkoa  unatarajiwa kuwa na ugeni mkubwa, ambapo baadhi ya wafanyabiashara wameanza kutumia fursa hiyo kwa kuboresha huduma mbalimbali, huku wengine wasio waaminifu wakijaribu kuongeza bei kwa lengo la kupata faida maradufu.
Kauli ya Dk. Christine imekuja kutokana na utafiti kuonyesha kuwa, hali ya maisha mkoani hapa imeanza kupanda, huku bidhaa mbalimbali zikipanda bei kwa kasi na kuwafanya wenyeji kuwa kwenye wakati mgumu tofauti na walivyozoea.
Katika uchunguzi wake, Uhuru imebaini kuongezeka kwa bei za vyumba katika nyumba za kulala wageni katika baadhi ya maeneo tofauti na zile za siku chache zilizopita.
Uchunguzi huo umebaini, chumba kilichokuwa kikilipiwa sh. 20,000 sasa kimepanda hadi kufikia sh. 40,000, huku vile vya sh. 30,000 vikipanda hadi sh. 50,000 na vile vya sh. 10,000 vikipanda hadi kufikia 20,000 na 25,000.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Christine alisema mkoa umeunda kamati maalumu kwa ajili ya kushughulikia malazi ili kuepusha upandaji holela wa bei hizo, jambo ambalo ni sawa na utapeli.
ìTumegundua watu wameanza kupandisha vitu holela, nyumba za kulala wageni zimeanza kupangishwa kwa bei kubwa kuliko kawaida, jambo hili si sahihi na halitavumiliwa, na atakayebainika atachukuliwa hatua kali kisheria,î alisema.
Mkuu huyo wa mkoa amewataka wamiliki wa nyumba za kulala wageni kuhakikisha nyumba zao zinakuwa na usalama wa kutosha.
Alisema kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo umejipanga kuhakikisha kuwa wageni watakaoingia wanaishi kwa usalama hadi wanapoondoka.
Aliwataka wakazi wa mkoa huo kuwa wakarimu na kuwasaidia wageni watakaokuwa mkoani hapa kwa kipindi chote.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyakazi wa nyumba za kulala wageni walisema bei za vyumba zimepanda kutokana na wingi wa wageni wanaotarajia kuwasili kuanzia leo.
ìTumeagizwa tupandishe bei za vyumba zaidi ya kukubali hatuna ujanja, mgeni akija mwenyeji anapona,î alisema mmoja wa wahudumu wa nyumba ya kulala wageni iliyopo eneo la Makorongoni mjini hapa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru