Tuesday 8 October 2013

Mgomo watikisa



NA KHADIJA MUSSA
MGOMO wa madereva na wamiliki wa mabasi uliodumu kwa saa tatu, ulisababisha hali kuwa tete katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani na Nchi Jirani cha Ubungo.
Mgomo huo ulioanza alfajiri, ulisababisha abiria kuwa katika wakati mgumu baada ya madereva kuruhusu abiria kupanda tayari kwa safari, kisha wenyewe kwenda kujificha mahali pasipojulikana.
Hata hivyo, kilichowakera zaidi abiria ni hatua ya wamiliki kukatisha tiketi kwa abiria ilhali wanafahamu kuwa wanaingia kwenye mgomo.
Kutokana na hatua hiyo, serikali iliwaonya wamiliki wa mabasi watakaoendelea na mgomo kuwa itafuta leseni za usafirishaji.
Abiria walilaani kitendo cha wamiliki na wafanyakazi wa mabasi hayo, jambo waliloliita kuwa uhuni na unyanyasaji mkubwa.
Waliitaka serikali kuhakikisha inachukua hatua kali kwa wamiliki na madereva waliogoma kwa uhuni huo, ambao haukubaliki.
Abiria hao ambao wengi walifika kituoni hapo kuanzia saa 11.00 alfajiri, walijikuta wakitelekezwa ndani ya magari hadi saa 2.48 asubuhi, baada ya serikali kutangaza onyo hilo.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga kutishia kufuta leseni kwa wamiliki wa mabasi na madereva watakaokaidi amri ya kusitisha mgomo.
Mgomo huo unafuatia ule wa malori ulioanza wiki iliyopita wakigomea ongezeko la tozo la asilimia tano katika vituo vya mizani.
Kufuatia mgomo huo, baadhi ya madereva wa teksi waliamua kufanya safari za mikoani, ambapo kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro ilikuwa kati ya sh. 300,000 hadi 500,000.
Kamanda Mpinga alilazimika kutoa agizo hilo baada ya mgomo uliofanywa na wamiliki wa mabasi ya mikoani kugomea magari yao kupimwa katika vituo vya mizao.
ìKwa kuwa wameingia mkataba wa kusafirisha abiria na tayari wameshachukua fedha za wananchi, wana wajibu wa kisheria wa kuwasafirisha, bila kufanya hivyo watakuwa wamevunja sheria,î alisema.
Kamanda Mpinga aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kituoni na kuongeza wamewasiliana na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), kuorodhesha mabasi yatakayoendelea na mgomo ili yafutiwe leseni.
Pia, Kamanda Mpinga alitumia fursa hiyo kuwataka madereva walio njiani kuegesha magari yao pembeni ili kupisha wengine waendelee na safari.
Akizungumzia kuhusu suala la upimaji wa mabasi hayo katika vituo vya mizani, alisema suala hilo litashughulikiwa na mamlaka husika, nao kuwaomba madereva hao kuendesha kwa umakini.
Naye, Mkurugenzi wa Barabara wa SUMATRA, Gield Ngewe alisema kitendo cha kukataa kutoa huduma ni kinyume cha taratibu za leseni, hivyo aliwataka kutoa huduma kabla ya kushushiwa rungu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa TABOA, Severin Ngallo alisema walikubaliana mabasi yote yaendelee kutoa huduma ila yasipime uzito katika vituo vya mizani.
Pia, aliwaomba abiria kutokata tiketi kwa ajili ya safari hadi hapo watakapotangaziwa, kwa kuwa bado wanaendelea na mazungumzo na serikali kuhusu maombi yao ya kutopima mabasi katika vituo vya mizani.
ìTatizo wanadhani tunafanya biashara ya kubeba mizigo, sisi tunabeba abiria tu, hivyo tunaomba serikali iondoe tozo hilo ya asilimia tano pamoja na upimaji, kwani katika nchi nyingine ambazo tunatoa huduma utaratibu huo haupo,î alisema.
Alisema iwapo serikali haitakubaliana nao kuhusu kuondoa utaratibu wa mabasi kupima uzito katika vituo vya mizani wataendelea kugoma.
Baadhi ya abiria waliokuwa wasafiri jana,  walisema kitendo kilichofanywa na baadhi ya madereva na wamiliki wa mabasi hayo si cha kiungwana.
Walisema kuwa hakukuwa na sababu za kukatisha tiketi wakati walijua kuwa walikuwa na mgomo, kwani ni bora wangefunga ofisi ili kuepusha usumbufu kwa abiria.
ìHuu ni uhuni na wizi... kwa nini wanaendelea kukatisha tiketi wakati wanafahamu kuwa wapo katika mgomo, ni lazima serikali ichukue hatua dhidi ya wote waliosababisha usumbufu huu,î alisema Alex Cosmas aliyekuwa akielekea Njombe.
Abiria walifika kituoni hapo alfajiri tayari kwa safari za kwenda mikoani, walikuwa hawajaondoka, kwani hadi saa 2.25 asubuhi, kulikuwa hakuna gari lolote lilitoka kituoni hapo, licha ya kuruhusiwa kupanda mabasi na kisha madereva kutokomea.
Ilipofika saa 2.45 asubuhi, Kamanda Mpinga aliwatangazia abiria kuingia katika mabasi waliyokata tiketi na kuwataka madereva wote kuanza safari mara moja.
Juzi, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema kinachofanywa na wizara yake ni kufuata sheria, na kwamba anayetaka kupinga, hana budi kupeleka malalamiko yake bungeni ili sheria iliyopo ibadilishwe, na si kwa kuandika barua wizarani kwake.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, ili sheria iweze kubadilishwa ni lazima bunge liridhie kubadilisha sheria hiyo na sio kwenye makaratasi.
“Sheria iliyopo inaruhusu mtu kuja kukata rufani kwa Waziri wa Ujenzi... kama ameona sheria iliyopo haifai na kama hakuridhika na uamuzi utakaotolewa anatakiwa aende mahakamani,” alisema Dk. Magufuli.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru