Thursday 24 October 2013

Mganga mbaroni kwa wizi wa dawa


Na Ahmed Makongo, Bunda
MGANGA Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk. Rainer Kapinga, anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za wizi wa sh. milioni 16 ambazo zilitengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa za binadamu.
Mbali na Dk. Kapinga, pia mtunza stoo wa halmashauri ya wilaya hiyo, aliyetajwa kwa jina la Mashini, naye anashikiliwa kwa tuhuma za kusababisha hospitali, vituo vya afya na zahanati kukosa dawa.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe, alisema Dk. Kapinga na Mashini walitiwa mbaroni juzi na wanahojiwa na polisi kuhusiana na wizi huo na watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bunda, Mika Nyange, alisema baada ya jeshi lake kupitia vielelezo vyote wahusika watafikishwa mahakamani.
Nyange alisema kukamatwa kwa Dk. Kapinga na Mashini, kunatokana na kutuhumiwa kuiba fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya kununua dawa za binadamu, lakini walizichukua kisha kuandika vielelezo bandia kuwa dawa hizo zimenunuliwa.
ìPamoja na maofisa hawa wawili ambao wanashikiliwa, lakini uchunguzi zaidi unafanyika katika taarifa ya mkaguzi wa hesabu za serikali, ili kuwakamata wote waliohusika katika mlolongo huo,îalisema OCD Nyange.
Naye Mirumbe alisema maofisa hao wanatuhumiwa kwa wizi wa fedha hizo ambapo inadaiwa walifanya uchakachuaji huo kati ya Machi hadi Juni, mwaka huu, na kwamba fedha hizo zinaonyesha kununua dawa hewa kupitia kwa mzabuni mmoja wa mjini hapa.
Kubainika kwa uchakachuaji huo ni kunatokana na Kamati ya Ulinzi na Usalama kubaini kuwepo kwa hali mbaya kwenye hospitali na kusababisha wagonjwa kukosa dawa.
Alisema wahusika wa uchakachuaji huo ni wengi na uchunguzi unaendelea kuwabaini wengine.
ìNi maeneo mengi kwenye vituo vya afya kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha na usimamizi mbaya wa idara ya afya...tutawakamata wote na kuwafikisha mahakamani, hatuwezi kuvumilia hali hii wakati wananchi wetu wanakosa dawa kwa tamaa ya watu wachacheî alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru