Thursday 17 October 2013

Wafukuzwa kijijini kwa uchawi, uzinzi


NA MARCO KANANI, CHATO
WANAKIJIJI wanane wakiwemo wanawake watano wa kijiji cha Mwendakulima wilayani hapa mkoani Geita, wamefukuzwa na mwenyekiti wa kijiji hicho baada ya kupigiwa kura ya kuwa wachawi na wazinzi. 
Tukio hilo lilitokea Oktoba mosi, mwaka huu, katika mkutano unaodaiwa kutokuwa wa kisheria ulioitishwa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Damian Moris akishirikiana na Mtemi wa Sungusungu wa kijiji, Dogita Nzwarile na Katibu wake, Agostine Mbapula.
Viongozi hao wanadaiwa kuendesha mchakato wa upigaji kura kwa watu wanaotuhumiwa kuwa wachawi na wazinzi kijijini hapo.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Levelian Lwekiga, alithibitisha kufanyika kwa mkutano huo usio halali, na kuongeza licha ya yeye kutohudhuria baada ya kubaini uvunjwaji wa sheria, alitoa taarifa kwa mamlaka husika, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
"Ni kweli mkutano huo ullifanyika na kitendo cha kuwataja hadharani wananchi kuwa ni wachawi ni kosa la jinai na linahatarisha usalama wao nakuchochea chuki kwa jamii. Mwenyekiti aliitisha mkutano huo kwa maslahi binafsi, kwani hana uwezo huo kisheria na hii ni mara yake ya pili kufanya hivyo," alisema Lwekiga.
Alikiri baada ya kutuhumiwa kutajwa hadharani, waliamriwa na mkutano huo ambao ulihudhuriwa na wanakijiji 60, wakati kijiji kina zaidi wakazi 3,400, hatua inayoashiria kuwepo kwa ajenda ya siri.
Wanakijiji waliokumbwa na mkasa huo ni Petro Mkwavi (80), Ndagalele Petro (40), Agnes Maduvungu (41), Agnes Kisulila (48), Leah Robert (35), Elizabeth Edward (46), Henriko Kisulila na Deus Luchenja, ambaye anatuhumiwa kuwa mzinzi.
Kwa upanda wake, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Damian Morice (CHADEMA), alikiri kuitisha mkutano huo akishirikiana na uongozi wa sungusungu na kwamba, aliombwa kufanya hivyo na wanakijiji licha ya mkutano huo kuhudhuriwa na watu wachache.
Hata hivyo, alidai kuwa mkutano huo ulikuwa halali na sheria haikukiukwa kwa kuwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Polisi Wilayani hapa zilikuwa na taarifa rasmi.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya, Rodrick Mpogoro ameelezea kusikitishwa na hatua hiyo na kuonya kuwa vitendo hivyo haviwezi kuvumiliwa.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Donald Nyahoga akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu, alikana na kuagiza wananakijii walioathiriwa kuripoti ofisini kwake ili hatua ziweze kuchukuliwa, kwani, kitendo hicho ni kosa la jinai licha ya kuhatarisha amani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru