Thursday 24 October 2013

Vigogo Namtumbo wabanwa mbavu


NA KHADIJA MUSSA
MWENYEKITI wa Kamati ya Hesabu za Serikali (LAAC), Rajab Mohammed Mbarouk, amemtaka Mwenyekiti wa Halmashauri ya Namtumbo mkoani Ruvuma kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kuacha kukidhoofisha Chama.
Pia, kamati hiyo imekataa taarifa ya hesabu ya halmashauri hiyo na kuiagiza kuifanyia marekebisho na kuirudisha tena mbele ya kamati Desemba mwaka huu.
Amesema kitendo cha kutosimamia fedha za maendeleo ya wanawake na vijana kinadhalilisha Chama chake (CCM) na kuhujumu jitihada za serikali.
Aliyasema hayo jana katika Ofisi Ndogo ya Bunge, Dar es Salaam wakati kamati hiyo ilipowahoji viongozi wa halmashauri hiyo ambapo, ilibaini kwa muda wa miaka mitatu mfululizo haijapeleka fedha hizo kwa wahusika hivyo kusababisha malalamiko makubwa.
Mbarouk alisema ni aibu kwa halmashauri hiyo kushindwa kufikisha fedha hizo kwa wahusika wakati serikali inazipeleka na wao kuzitumia kwa matumizi mengine.
Naye Azza Hamad (Viti Maalumu CCM), alisema hayupo tayari kuona CCM kikidhalilishwa hivyo, aliomba kamati ya nidhamu kulishughulikia suala hilo.
Alisema wamechoshwa na vitendo vya baadhi ya halamashauri kushindwa kusimamia ipasavyo fedha za maendeleo zinazotolewa na serikali na badala yake kuishia katika matumizi ya posho za wataalamu.
Kutokana na hilo, Mwenyekiti wa kamati hiyo alimuagiza mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuhakikisha anasimamia ulipaji wa madeni hayo na suala la maendeleo ya vijana na wanawake linakuwa moja ya ajenda katika vikao vyao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru