Tuesday, 1 October 2013

Waandamana kwa kukosa mikopo



NA JUMANNE GUDE
BAADHI ya wanafunzi waliokosa mikopo ya elimu ya juu, wameandamana hadi Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kujua hatima yao.
Mikopo hiyo hutolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).
Wanafunzi hao walieezea kilio chao baada ya kukosa mikopo, licha ya kutimiza masharti.
Baada ya kuhoji sababu za kunyimwa mikopo, hawakupewa majibu na badala yake walipigwa danadana.
Wanafunzi hao, walidai kuwa wameamua kuandamana kwa sababu wao ni yatima na na wengi wao wamechaguliwa katika fani za sayansi na elimu, ambao kimsingi, wanahaki ya kupewa mikopo.
Mmoja wa wanafunzi hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Frank, alisema wanataka kuonana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, ili kujua hatima yao.
“Tuliuenda bodi ya mikopo, lakini hawakutusikiliza, ndio maana tuko hapa wizarani ili kujua hatima yetu.
“Tulistahili kupata mikopo na endapo bajeti haikutosha, tungeelezwa,” alisema Frank.
Hata hivyo, hawakuweza kumona waziri na badala yake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha wizara hiyo, Ntambi Bunyazu, alisema Wizara imewasikiliza na kuwarudisha bodi ya mikopo ili suala lao likapatiwe ufumbuzi huko.
“Kila mtu amekuja na tatizo lake, tumezungumza nao na tumewaambia warudi bodi ya mikopo, suala lao litashughulikiwa huko ili kila mtu apate haki,” alisema.
Bunyazu, alisema bodi ya mikopo itawaelekeza namna ya utoaji mikopo na sababu za kupewa au kutopewa na endapo hawataridhika, wana haki ya kukata rufani.



Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru