Thursday, 24 October 2013

Pinda ainadi Tanzania kwenye maonyesho



na mwandishi wetu, China
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amewaeleza washiriki wa Maonyesho ya 14 ya Kimataifa ya China Magharibi, kuwa Tanzania ni nchi ya pili duniani na ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na vituo vingi vya utalii na akawataka waanze kumininika kwa wingi kuja nchini kutalii.
Alitoa mwaliko huo jana wakati akihutubia kwenye maonyesho hayo yanayojulikana kama ‘14th Western China International Fair’ yaliyoanza jana jijini Chengdu kwenye jimbo la Sichuan, China na kuhudhuriwa na mataifa mbalimbali.
Waziri Mkuu Pinda, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa mataifa 11 waliopata fursa ya kuhutubia maonyesho hayo makubwa, aliziomba kampuni za China kuja nchini kuwekeza kwa kujenga viwanda vya nguo zinazotokana na zao la pamba lilimwalo nchini.
Alitumia fursa hiyo pia kuinadi Tanzania kuwa ni nchi yenye ardhi kubwa tena yenye rutuba ambayo inafaa kwa kilimo, na kuzisihi kampuni za Kichina ambazo zinataka kuwekeza kwenye sekta ya kilimo, zije nchini.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu Pinda aliwaambia wawakilishi wa kampuni mbalimbali za kimataifa zinazoshiriki kwenye maonyesho hayo kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazolima pamba kwa wingi wakati China ni taifa ambalo limebobea kwa viwanda.
“Sisi tuna pamba na ninyi mna viwanda, nawaomba mje nchini kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya nguo kwani malighafi ipo ya kutosha,” alisema Pinda. Maonyesho hayo yanashirikisha kampuni 4,000 kutoka nchi 72 ulimwenguni na majimbo mengine ya China.
Ufunguzi wa  maonesho hayo ulihudhuriwa na wakuu wa nchi saba, mawaziri wakuu wanne akiwemo Pinda, mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi 25, wakuu wa mashirika ya kimataifa tisa na mabalozi wanane wanaoziwakilisha nchi zao nchini China.
Akizungumzia kuhusu utalii,  Waziri mkuu alisema Tanzania ni nchi ya pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki yenye vivutio vingi vya utalii vikiwemo vitatu vilivyoko kwenye maajabu saba ya Afrika.
“Kati ya maajabu saba mapya ya asili barani  Afrika yaliyotangazwa Februari, mwaka huu, maajabu matatu yako nchini kwetu, ambayo ni mlima Kilimanjaro, hifadhi ya Serengeti na Bonde la Ngorongoro,” alisema na kuongeza kuwa pamoja na vivutio hivyo lukuki, bado idadi ya watalii wanaofika nchini kutoka China haijawa ya kuridhisha.
Alisema licha ya maajabu hayo matatu, pia kuna hifadhi nyingine za wanyama, hifadhi za mambo ya kale na kisiwa maarufu cha Zanzibar.
Alisema hata takwimu za kimataifa zinaitaja Tanzania kama nchi ya pili duniani yenye vivutio vingi kuliko nchi zingine ikiifuatia Brazil ambayo inaongoza kwa vivutio duniani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru