Wednesday, 30 October 2013

Mama wa mtoto aliyeathirika akili adai kutishwa


NA RABIA BAKARI
SAKATA la mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Newala mkoani Mtwara, Salim Shamte, kudaiwa kuathirika akili kutokana na kipigo cha mwalimu wake, limechukua sura mpya.
Shamte anadaiwa kupigwa na mwalimu wake wa darasa, Fredrick Kapinga, kwa kile kilichoelezwa kuwa deni la sh. 300 alilotakiwa kulipa baada ya wanafunzi wa darasa hilo kupoteza vitabu viwili.
Hatua hiyo imetokana na mama wa Shamte, Vena Lupaso, kuanza kupokea vitisho kwa lengo la kumnyamazisha asiweze kupaza sauti kudai haki.
Kwa wiki kadhaa sasa, gazeti hili limekuwa likiripoti tukio hilo, ambapo juzi usiku, Vena alipokewa simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Akizungumza na gazeti hili jana, Vena alisema ofisa huyo wa TAKUKURU, alijitambulisha kwa jina la Eva Mushi na kumweleza kuwa, wamekuwa wakimuona akilalamika katika vyombo vya habari na kumtaka aache kufanya hivyo.
Alisema ofisa huyo alimtaka kwenda katika Bodi ya Shule ili aweze kupatiwa msaada badala ya kulalamika na kuahidi kuwa yeye na maofisa wenzake wa TAKUKURU watamtafuta ili kuzungumzia suala hilo na namna ya kulipatia ufumbuzi.
"Aliponipigia alijitambulisha kwa jina la Eva Mushi, hivyo alipokata simu niliangalia jina la mmiliki wa namba hiyo na kukuta imesajiliwa kama Suzana Kapinga, nikagundua kuna mchezo mchafu nimeanza kufanyiwa," alisema.
Alisema, baada ya kukumbwa na wasiwasi huo, akihofiwa mwanaye kuwa anaweza kudhurika zaidi, alikwena kutoa taarifa kituo cha polisi kwa hatua zaidi.
"Jana (juzi), nilienda Kituo cha Polisi Tabata, na kupewa RB namba TBT/RB/3068/2013, ikiwa kuna jambo lolote litaendelea," alisema.
Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Zelothe Steven alisema bado anafuatilia suala hilo na atalitoa tamko.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru