Wednesday, 9 October 2013

Mfanyabaishara Arusha amwagiwa tindikali



NA LILIAN JOEL, ARUSHA
MFANYABIASHARA Japhet Minja (30), amelazwa katika Hospitali ya Selian mjini hapa, baada ya kumwagiwa tindikali usoni na watu wasiojulikana.
Minja alipatwa na mkasa huo jana, saa 12.15 asubuhi, eneo la Shamsi, wakati akitoka nyumbani kwake kwenda kazini.
Akizungumzia tukio hilo ambalo limezua taharuki kubwa jijini hapa, mmoja wa ndugu wa Minja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema Japhet alipatwa mkasa huo akiwa ndani ya gari lake katika eneo hilo.
ìMinja alipofika eneo la Shamsi alikutana na vijana wanne wakiwa wamesimama kando ya barabara wakamsimamisha kama vile watu waliokuwa wakiomba msaada... baada ya ndugu yangu kusimama na kushusha kioo cha gari upande wake, ghafla watu hao wakafungua mlango kwa nguvu na kumtoa ndani ya gari na kumpiga kisha kumwagia tindikali usoni,î alisema.
Alisema baada ya Minja kumwagiwa tindikali, wasamaria wema waliokuwa wanasubiri daladala katika eneo hilo walimchukua na kumpeleka katika Hospitali ya Rufani ya Selian, huku vijana hao wakikimbilia kusikojulikana.
Baada ya tukio hilo, waandishi wa habari walifika  hospitalini hapo kumwona Minja, lakini uongozi wa hospitali uligoma kuzungumzia chochote kwa madai kuwa, hali ya mgonjwa ni mbaya na amelazwa katika Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU).
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Liberatus Sabas alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kwamba polisi inaendelea na uchunguzi kuhusiana na shambulio hilo.
Kwa mujibu wa Sabas, uso wa Minja umeathirika kiasi, lakini pia alingíatwa kidole cha mkono wa kulia na watu hao waliomshambulia.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru