Wednesday, 9 October 2013

JK aweka rehani nafasi za Ma-RC





NA SELINA WILSON
SERIKALI imewatangazia kiama wakuu wa mikoa na wilaya watakaoshindwa kutekeleza agizo la kujenga maabara katika shule za sekondari ifikapo Novemba, mwakani.
Imesema kwa watakaoshindwa watakuwa wamejiweka kwenye mazingira magumu ya nafasi zao.
Rais Jakaya Kikwete alisema hayo jana, wakati akihutubia, maelfu ya wananchi waliofurika katika Uwanja wa Polisi mjini Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Alisema hatokuwa na msalie mtume kwenye agizo hilo ambalo alilitoa mwaka jana, na kuongeza kwa atakeyeshindwa ajue atakuwa kwenye hali ngumu.
ìNataka wakuu wa mikoa na wilaya, mchemke mfanye kila linalowezekana ili kuhakikisha maabara zinajengwa, sitaki kusikia malalamiko, mmepewa kazi chemkeni mambo yaonekane,î alisema.
Alisema ujenzi wa maabara moja ni kati ya sh. milioni 45 hadi 50, na kwamba sekondari zinahitajika maabara mbili hadi tatu.
Aliwataka viongozi hao wasisubiri kukumbusha ahadi za Rais tu, kwani yapo mambo mengine ni maelekezo ya Rais na kwamba watekelezaji ni viongozi hao kwa kushirikiana na halmashauri zao.
Rais Kikwete alisema serikali inaendelea kuboresha sekta ya elimu kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo nyumba za walimu na upatikanaji wa walimu, lakini kwenye maabara maelekezo yalishatolewa, na kwamba kinachotakiwa ni utekelezaji.
“Tumeshazipatia sh. milioni 500 kila halmashauri, ili kujenga nyumba za walimu, ninachotaka fedha hizo zisimamiwe vizuri ili malengo hayo yafikiwe,” alisema.
Kuhusu walimu, alisema kwa mwaka huu walimu 18,000 wataajiriwa kwenye shule za sekondari na wengine 18,000 shule za msingi, kwani lengo ni kuhakikisha sekta ya elimu inakwenda vizuri.
Kabla ya kuanza kuhutubia, Rais Kikwete, alimsimamisha Diwani wa Kata ya Chalinze, Nasser Karama aeleze kero za wananchi wa eneo hilo, ambapo alizitaja kuwa stendi ya mabasi, umeme kwa baadhi ya vijiji ambavyo havipo kwenye mpango wa vijiji 20 na hospitali kubwa.
Akijibu kero hizo, Rais Kikwete alisema serikali yake itashirikiana nao bega kwa bega, ila waanze mchakato wa kutenga maeneo na kuhusu umeme litafanyiwa kazi.
Aliwataka watenge eneo nje ya eneo la makutano ya barabara za Morogoro na ile ya Chalinze/Segera, kwani wanatakiwa kuungalia mji wa Chalinze kwa siku za baadaye na si kwa matumizi ya sasa tu.



Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru