Tuesday 1 October 2013

Japan yatoa msaada wa mbolea


RACHEL KYALA
MATUMIZI ya mbolea yatasaidia jitihada za serikali katika mpango wa kuleta tija kwenye sekta ya kilimo nchini.
Sekta hiyo huchangia asilimia 15 ya pato la taifa.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Injinia Christopher Chiza, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipokea msaada wa mbolea kutoka serikali ya Japan.
Alisema mbolea hiyo itasambazwa kwa wakulima, hususan wale wa kipato cha chini kwa bei nafuu, ili kupunguza umaskini na kuboresha usalama wa chakula nchini.
“Hapo awali tulipokea misaada mingi ya mchele toka serikali ya Japan, lakini tuliona ni bora watuwezeshe kwenye kilimo cha mpunga ili kuepuka kuomba msaada mara kwa mara,’’ alisema Chiza.
Waziri Chiza, alisema msaada uliotolewa  ni wa mbolea aina ya DAP tani 6,003 yenye tahamani ya sh. bilioni 16.7.
Aliahidi kuwa itatumiwa vizuri ili kufikia malengo ya matokeo makubwa sasa (BRN).
Pia, Waziri huyo aliishukuru serikali ya Japan kwa kuisaidia Tanzania kuimarisha  kilimo cha umwagiliaji, ambapo Mei, Mwaka huu, ilikabidhi msaada wa takribani sh. bilioni 54 ili kukiboresha .
Akikabidhi msaada huo, Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada, alisema lengo kuu ni kusaidia kuongeza uzalishaji wa chakula kwa wakulima wa kipato cha chini nchini, na kuongeza usalama wa chakula na kupunguza umasikini.
“Tumekusudia pia kuendeleza mradi wa kilimo cha mpunga huko Mpiji, pamoja na kuongeza tija katika kilimo cha umwagiliaji na kuboresha miundombinu yake,’’ alisema.
Okada, alisema lengo la serikali yao kutoa misaada ya mara kwa mara kwa Tanzania ni kudumisha uhusiano kati ya nchi mbili hizi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru