Tuesday 29 October 2013

Watano wanaswa na mkono wa binadamu


Mwanza, waganga wa kienyeji
NA PETER KATULANDA, MWANZA
WATU watatu wakiwemo waganga wawili wa kienyeji, wametiwa mbaroni kwa kukutwa na kiungo cha mkono wa kulia wa binadamu, wakiwa kwenye harakati za kukiuza.
Watuhumiwa hao walikamatwa juzi, saa tisa alasiri, katika eneo la kati ya ufukwe wa Ziwa Victoria na Uwanja wa Ndege wa Mwanza, kutokana na taarifa za raia wema, ambapo polisi waliweka mtego kama wanunuzi na kufanikiwa kuwanasa.
Habari za kuaminika zinasema, miongoni mwa watuhumiwa hao yumo mfanyabiashara maarufu jijini hapa, ambaye amekuwa akishirikiana na waganga kufanya biashara hiyo haramu.
Habari zilizothibitishwa na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, Joseph Konyo, watuhumiwa walipokuwa wakikinadi kiungo hicho waliwaeleza wanunuzi (polisi) kuwa wana kila aina ya viungo ambavyo watahitaji.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa, Ernest Mangu,, Konyo alivitaja baadhi ya viungo vya binadamu ambavyo watuhumiwa hao walidai wanavyo kuwa miguu, kichwa na sehemu za siri za mwanamke au mwanamme.
Alisema kabla ya kunaswa, mchakato wa biashara hiyo ulichukua takriban wiki mbili na wauzaji walitaka kupatiwa sh. milioni 100 kwa kiungo kimoja, ambapo walitakiwa kupunguza kidogo, ikiwa ni pamoja kuonyesha kiungo hicho na kupanga eneo mwafaka la kufanyika kwa biashara hiyo.
“Kiungo hicho kilikuwa bado kibichi kabisa na ni cha binadamu, walikihifadhi kwenye begi ambalo ndani yake ulikuwa umewekwa kwenye mfuko wa Rambo uliofungwa kwa ustadi mkubwa,’’ alisema Konyo.
Hata hivyo, polisi walipata wakati mgumu kudhibiti baadhi ya wananchi waliokuwa jirani na eneo hilo, ambao walishtushwa na tafrani ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Wananchi hao walitaka kuwashambulia na kuwaua watuhumiwa hao baada ya kugundua walikuwa na kiungo cha binadamu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru