Thursday, 31 October 2013

Watahiniwa kidato cha nne watajwa


NA SELINA WILSON
WATAHINIWA 427,906 wanatarajiwa kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne, utakaoanza Novemba 4 hadi 21 mwaka huu.
Kiasi hicho ni pungufu ya watahiniwa 53,508 sawa na asilimia 11.1, ikilinganishwa na watahiniwa waliojiandikisha kufanya mtihani huo mwaka jana, waliokuwa 481,414.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alisema kati watahiniwa hao, 367,399 ni wa shule za sekondari na 60,507 wanajitegemea.

Alisema kati ya watahiniwa hao, wamo 39 wasioona kati ya 309 wenye uono hafifu ambao wanahitaji maandishi makubwa, ingawa maandalizi yake yamekamilika.
Profesa Mchome alisema kati ya watahiniwa wa shule ya sekondari 198,257 sawa na asilimia 53.96 ni wavulana na wasichana ni 169,142 sawa na asilimia 46.04.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, wasichana ni 30,051 sawa asilimia 49.67 na wanaume ni 30,456 sawa na asilimia 49.67, na kwamba kati yao watahiniwa 18,214 wamejiandikisha kufanya mtihani wa maarifa.
Alisema mtihani huo wa kidato cha nne utafanyika katika shule za sekondari 4,365, vituo 923 vya kujitegemea na vituo 636 vya watahiniwa wa Maarifa (QT).
Akizungumzia maandalizi ya jumla, Profesa Mchome alisema usafirishaji wa mitihani hiyo hadi kwenye ngazi ya mkoa yamekamilika, na kwamba mikoa inaendelea na utaratibu wa kuhakikisha kila kituo kinapata mitihani yake kwa kuzingatia muda ulipangwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).
Kuhusu usalama, katibu mkuu huyo alisema hadi sasa hali ni shwari, na kwamba hakuna mtihani uliovuja katika ngazi yoyote, hivyo aliipongeza NECTA kwa kufanikisha maandalizi hayo.
Profesa Mchome aliwataka walimu na wasimamizi wa mitihani kuzingatia utaratibu kama walivyoelekezwa katika semina bila kuwatisha watahiniwa, na kwamba watakaojihusisha na udanganyifu katika mitihani watachukuliwa hatua stahiki.
Aliwataka wazazi, viongozi na jamii kushirikiana  ili kuhakikisha mtihani huo unafanyika katika mazingira salama, tulivu na amani na wakuu wa shule wahakikishe mahitaji yote muhimu yanapatikana.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru