NA RABIA BAKARI
MWANAFUNZI wa Kidato cha Pili katika Sekondari Newala, mkoani Mtwara, Salim Shamte, amepata ulemavu wa akili kwa madai ya kipigo kutoka kwa mwalimu wake.
Mateso kwa mwanafunzi huyo, ambaye alikuwa na ndoto nyingi katika maisha yake, yametokana na deni la sh. 300, ambazo alitakiwa kulipa kufuatia kupotea kwa vitabu darasani kwao.
Tukio hilo, lilitokea Oktoba Mosi, mwaka huu, ambapo mwalimu huyo Fredrick Kapinga, alikuwa akikusanya sh.300 kwa wanafunzi wa darasa analosoma Salim, kama adhabu ya kupoteza vitabu viwili vya shule.
“Alipofika kwa Salim, alimjibu kuwa hakuwepo siku ambayo vitabu vinapotea, na mwalimu alimjibu kuwa anafahamu waliopoteza ni wachache, lakini adhabu hiyo italikumba darasa zima.
“Alimjibu ‘haya mwalimu nitalipa’, na ndipo mwalimu alipomkunja na kuanza kumpiga kwa nguvu na kumvutia nyuma ya darasa ambapo, alimbamiza ukutani mara mbili kisha kumweleza arudi akapige magoti na wenzake mbele ya darasa,” alisema mlezi wa mwanafunzi huyo, Neema Solo.
Baada ya tukio hilo, mwanafunzi huyo alianza kuumwa kichwa na kupiga kelele, walipokwenda shuleni kufahamu kilichompata, Mwalimu Kapinga, alikiri na kuomba samahani, kwamba alipandwa na hasira baada ya kujibiwa ‘haya’ badala ya sawa, ambapo aliona amedharauliwa.
“Nilipata taarifa kuwa hali ya mtoto wangu ni mbaya, nikapanda basi na kwenda Newala, ambako nilimkuta mahututi, tuliandikiwa fomu namba tatu ya matibabu kutoka Polisi (PF3), na mwalimu alishikiliwa na polisi,” aliongeza mama wa mtoto huyo, Vena Lupaso mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Alisema kutokana na hali ya mtoto kuzidi kuwa mbaya, waliandikiwa rufani kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili, kitengo cha wagonjwa wa mifupa, ambapo aliendelea na matibabu.
“Cha kushangaza tukiwa kule Newala hospitali, kuna taarifa ilienda kwa polisi kwamba mtoto anaendelea vizuri na mwalimu Kapinga akaachiwa ndani ya siku moja, na hata PF3 ya mwanzo ilipotezwa, ndipo tukaandikiwa nyingine baada ya kuomba,” alisema Vena.
Kwa mujibu wa Vena, hata mwalimu huyo kukamatwa na polisi ni kwa msukumo wa wanafunzi ambao, walishuhudia tukio hilo, na kutoa ushirikiano mkubwa kwa mwenzao.
Mtoto huyo kwa sasa hawezi kuzungumza vizuri na pia amepoteza kumbukumbu.
“Hapa unapomuona ni afadhali, kwani amepoteza kumbukumbu na madaktari walisema ni kilema cha muda mrefu kwani, hata kama atapona bado kunaweza kuwa na tatizo kwenye akili,” alisema Vena.
Ripoti za hospitali, zinaonyesha kuwa ubongo wa mtoto huyo umetikisika na itachukua muda mrefu kurudi katika hali ya kawaida.
Daktari kutoka Newala, ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alikiri kumpokea mtoto huyo katika hali mbaya, ambapo mwanzo walidhani amepasuka kichwani au ubongo umeingiliana na damu.
“Lakini baada ya vipimo, tulimshukuru Mungu, hatukuona matatizo tuliyodhani, lakini kutokana na ufinyu wa vipimo na ukubwa wa tatizo, tukaona wenzetu wa Muhimbili, watasaidia zaidi,” aliongeza.
Jana, gazeti hili lilikutana na jopo la madaktari wanaomtibu mtoto huyo, ambapo waliotoa maelekezo ya kuendelea na matumizi ya dawa mfululizo na kumpumzisha ili matibabu yawe rahisi.
Hata hivyo, walikataa kuzungumzia lolote na kwamba, ripoti itatoka kwa vibali maalum ama kwa kutakiwa na mahakama au polisi.
Mkuu wa Sekondari ya Newala, Babu Mshamu, alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini alisema limeshafika kwa Ofisa Elimu wa Newala, Alice Msemwa, ambaye alipotafutwa alidai yupo safarini.
Vena aliomba mamlaka zinazohusika kumsaidia ili sheria ichukue mkondo wake ikiwa ni pamoja na Mwalimu Kapinga kulipia gharama za matibabu, na mtoto arejee shuleni pindi atakapopata nafuu.
“Yeye alikuwa akidai sh. 300, lakini amesababisha madhara makubwa kwa mwanangu, hapa nilipo ni mjane, mtoto huyu nalea mwenyewe, nimesimamisha kazi zangu zote za kuniingizia kipato kumuangalia mgonjwa,” alilalama Vena.
Thursday, 24 October 2013
Mwanafunzi apata ulemavu kwa kipigo
08:09
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru