Na Mwandishi Wetu, Iringa
RAIS Jakaya Kikwete, amefurahishwa na kukoshwa na kazi nzuri inayofanywa na Kampuni ya Uhuru Publications Limited (UPL).
Alisema hayo juzi alipotembelea banda la UPL katika kilele cha kuzima mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofikia kilele katika uwanja wa Samora mjini Iringa.
UPL ndiyo wachapishaji wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo, Uhuru Wikiendi na Burudani.
Akiwa katika banda hilo, Rais Kikwete alisema amefurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na UPL, na kwamba ataviunga mkono vyombo vya Chama, kutokana na kazi nzuri ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha umma.
Mapema, wakati akiingia kwenye banda hilo na kupokelewa na mmoja wa wahariri, Bakari Mnkondo, Rais Kikwete alisikika akisema; “Hapa ndiyo nyumbani, hongereni sana.”
Pia, alivutiwa na picha za zamani zilizokuwepo, zikiwemo zinazoonyesha enzi za ujana wake.
“Mke wangu (mama Salma) njoo uone nilivyokuwa zamani, nilikuwa bado wamo,” alisema.
Baada ya Mama Salma kuona picha hizo, alionyesha kuzifurahia, huku akisema: “Hadi sasa, bado wamo”.
Viongozi wengine waliopita na kuchukua nakala ya gazeti la Uhuru lililoweka rekodi ya kuchapisha kurasa 136 ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Gazeti hilo lililochapishwa juzi, lilikuwa toleo maalumu kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Aidha, toleo hilo maalumu lilihusu kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, ambapo mwaka huu unatimiza miaka 49 tangu ulipoanza kuwashwa mwaka 1964 na Wiki ya Vijana.
Katika sherehe hizo, UPL pamoja na redio Uhuru Fm ilikuwa na banda maalumu lililokuwa na picha za waasisi wa Taifa letu, pamoja na wahariri na watumishi wengine wakielezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na vyombo hivyo vya Chama.
Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere, kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na Wiki ya Vijana zilifikia kilele juzi, kwenye uwanja wa Samora mjini hapa.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru