Tuesday, 8 October 2013

Mgambo wapigwa, wanusurika kifo


NA DUSTAN  NDUNGURU, MBINGA.
MGAMBO wanne na ofisa mtendaji wa kijiji cha Lipilipili wamenusurika kufa baada ya kushambuliwa na wananchi wakiwa kwenye majukumu yao ya kazi.
Vurugu hizo zilitokea juzi wilayani hapa na kudumu kwa saa tano, baada ya mgambo na ofisa huyo kufika kijijini hapo kwa ajili ya kuhudhuria kikao cha kamati ya maendeleo ya kata hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ,ofisa mtendaji wa kata ya Mpepai, Ansila Kumburu, alisema kikao cha kamati hiyo kilichokutana katika kijiji cha Luhangai, Septemba 27, mwaka huu, kiliamua wananchi waliokataa kuchangia shughuli za ujenzi wa maabara na bweni katika Shule ya Sekondari Dk. Ali Mohammed Sheni, wakamatwe na kuchangia sh. 25,000 kila mmoja.
Alisema kikao hicho kilikuwa chini ya mwenyekiti wake ambaye ni diwani wa kata hiyo, Francis Nchimbi, na kwamba aliamua kuleta mgambo ili kusaidia kuwasaka waliokataa kuchangia miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Kumburu, Septemba 30, mwaka huu, mgambo hao kwa kushirikiana na maofisa watendaji wa vijiji vya kata ya Mpepai, walianza kutekeleza agizo hilo kwa kupita kila kaya na kukusanya michango.
Alisema juzi katika kijiji cha Mtukula, mgambo tisa wakiwa na ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Petro Mayowa, walishambuliwa na wananchi.
Kumburu alisema katika vurugu hizo, Mayowa na mgambo hao walishambuliwa sehemu mbalimbali kwa kutumia silaha za jadi.
Alisema baada ya tukio hilo, wananchi walimchukua Mayowa na kumpeleka ofisini kwake na kumfungia ndani akiwa anavuja damu nyingi kichwani.
Kumburu aliwataja baadhi ya mgambo waliojeruhiwa katika tukio hilo kuwa Loy Mbunda, Joseph Alli, Kanisius Ngonyani, Agnes Mwilafi na walipatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Mbinga.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Robert Elisha, alithibitisha kupokea majeruhi hao, ambao hata hivyo walipatiwa matibabu na kuruhusiwa.
Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Deusdedit Nsimeki alisema watu wanane wanashikiliwa wakihusika na vurugu hizo.
Alisema watuhumiwa hao ni Bonventure Kapinga, John Nchimbi, Kondrad Haule, Wilson Kapinga, Thomas Kapinga, Maiko Kapinga, Zackaria Ndunguru na Amos Ndunguru.
Nsimeki alisema katika vurugu hizo, wanakijiji hao walitumia mapanga, magongo na fimbo za mianzi kuwashambulia mgambo hao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru