NA FURAHA OMARY
WAKILI Mabere Marando, amedai Mahakama ya Rufani, iliteleza kisheria katika uamuzi wake ambao uliwatia hatiani na kuwahukumu kifungo cha maisha mwanamuziki Nguza Vikings au 'Babu Seya' na mwanawe Johnson Nguza 'Papii Kocha'.
Wakili huyo, alidai hayo wakati wa kusikilizwa kwa maombi ya mapitio ya hukumu hiyo, iliyotolewa Februari, 2010, Jopo hilo liliwatia hatiani Babu Seya na mwanawe Papii na kuwapa adhabu ya kifungo cha maisha. Jopo hilo liliwaachia huru watoto wengine wa Babu Seya, Nguza Mbangu na Francis Nguza.
Marando alidai mahakama hiyo ilijiridhisha kulikuwa na makosa katika kupokea ushahidi wa watoto na kwa sababu matakwa ya sheria hayakufuatwa hivyo ushahidi huo ulipaswa kufutwa na waleta maombi kuachiwa.
"Mlikubaliana na sisi kwamba Mahakama ya Kisutu ilikosea haikuzingatia uchukuaji wa ushahidi lakini mlisema ilimradi kuwe na ushahidi wa kuunga mkono. Sisi tulisema hapana,"alidai.
Pia, alidai mahakama hiyo, ilikosea katika hukumu yake kwa kusema kuna shahidi wa 13 aliyedai kwenye nyumba ya Babu Seya kuna mlango wa siri ambao mtu anaweza kuingia na asionekane, ushahidi ambayo haupo na wala shahidi huyo hakusema hivyo.
"Mashahidi walisema wao waliona katika nyumba ya Babu Seya kuna milango miwili wa mbele na nyuma na yote inainghia sebuleni, mtu huwezi kuingia katika chumba chochote bila kupitia sebuleni
"Sasa katika ukurasa wa 38 wa hukumu yenu, mmetamka kwamba shahidi wa 13 aliiambia mahakama kuna mlango fulani wa kuingia katika nyumba bila ya mtu mwingine kukuona. Ushahidi huo haupo katika ushahidi wa shahidi wa 13 hawakusema. Haya ndiyo mambo yanayojidhihirisha kuna kuteleza," alidai Marando.
Aidha, alidai katika ushahidi wa mashahidi wanaohusika na ushahidi uliowatia hatiani Babu Seya na Papii Kocha, walidai walikuwa wakiingia katika nyumba hiyo wakitokea dukani kwa Mangi ambaye alikuwa akijua kinachotokea.
Marando alidai kwa mujibu wa sheria, upande wa Jamhuri ulipaswa kumleta Mangi ambaye ni shahidi muhimu ili aje kuthibitisha, lakini katika hukumu yao walisema upande huo una hiari wa kumuita shahidi wanayemtaka, kauli ambayo ni kinyume cha sheria.
Alidai kuna kijana anaitwa Size ambaye anadaiwa alikuwa anawakusanya watoto wa kike na kuwapeleka kwa Babu Seya na kufanya kinachodaiwa kutendeka, lakini hakuitwa na wala mahakama hiyo katika hukumu haye haimkumzungumzia.
Hoja nyingine, Marando anadai mahakama hiyo, iliteleza kwa kutotoa maoni yake juu ya utetezi wao, kuhusu uwepo wa watu katika nyumba ya Babu Seya, ambao walidai ingekuwa si rahisi watoto kuingia bila ya wao kuwaona kwa kuwa kuna milango miwili ambayo inaingia sebuleni.
"Naomba mpitie tena hukumu yenu na kurekebisha mambo ninayoona yana makosa ya kiuterezi na mkikubaliana nasi mfute washitakiwa kutiwa hatiani na mfute adhabu zao," aliomba Marando.
Upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Jackson Bulashi, akishirikiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Mwangaza Mwipopo, Emmaculata Banzi, Joseph Pande na Wakili wa Serikali Apimaki Mabrouk.
Wakili Bulashi aliiomba mahakama hiyo, kutupilia mbali maombi hayo kwa sababu yalishatolewa uamuzi katika rufani waliyokata waleta maombi. Alidai kwa upande wao wanaona hakuna makosa yaliyofanywa katika kufikia uamuzi huo na kwamba kilichowasilishwa ni sababu za rufani ambazo tayari zilishatolewa uamuzi.
Jopo la Majaji lilisema kuwa limesikia hoja za pande zote na kwamba wataarifiwa tarehe ya kutolewa uamuzi. Awali, jopo hilo lilitupilia mbali maombi ya mapitio yaliyokuwa yamewasilishwa na Babu Seya na Papii Kocha mwenyewe kwa msaada kutoka gerezani, kwa kuwa hawakutumia vifungu sahihi kuyawasilisha.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru