Thursday 17 October 2013

Ndugu wa mume waja na mapya


NA JESSICA KILEO
FAMILIA ya aliyekuwa mzazi mwenzake, Mwandishi wa ITV na Radio One, Ufoo Saro, Anthery Mushi (40), imevunja ukimya na kudai inapata wakati mgumu kuamini kwamba ndugu yao alijiua mwenyewe. 
Imesema suala hilo inaliachia Jeshi la Polisi lishughulikie ili kubaini undani wake.
Kaka wa marehemu, Isaya Mushi alidai hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wawakati mwili wa Mushi, aliyejiua kwa kujipiga risasi na kumuua mama mkwe wake, Anastazia Saro pamoja na kumjeruhi mchumba wake Ufoo, ukiagwa.
Mushi alidai wapo katika wakati mgumu wa kuamini kwamba ndugu yao alijiua mwenyewe, kwani haiwezekani mtu akajipiga risasi sehemu mbili ambazo ni kidevuni na upande wa bega la kushoto.
Alidai sio kazi yao kutoa hukumu, kwani wanasubiri upelelezi wa polisi kutoa jibu lililo sahihi kuhusiana na tukio hilo.
Baada ya kifo cha ndugu yetu, wanafamilia tulifanya uchunguzi wa awali na bado linatuwia vigumu kutambua upi ni ukweli kuhusu jambo hilo kuhusiana na kifo hiki,î alidai.
Kaka huyo alidai katika uchunguzi wa madaktari, walibaini kuwa marehemu alijipiga risasi mbili sehemu tofauti.
Akisoma risala kwa waombelezaji, Mushi alidai marehemu alizaliwa Januari 3, 1973 katika kijiji Uru Ongoma Timbirini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mushi alisema alisoma Shule ya Msingi Ongoma Timbirini kutoka mwaka 1981 hadi 1987 na alijiunga na Shule ya Sekondari ya Zanzibar na baadaye alisoma kozi mbalimbali, ikiwemo uandishi wa habari.
Alisema mwaka 1994 alijunga na Kituo cha Televisheni cha ITV na mwaka 2002 alikwenda STR na hadi mauti inamkuta alikuwa akifanya kazi Umoja wa Mataifa, Sudan, akiwa mtaalamu wa habari.
Kwa upande wake, dada wa marehemu, Eviolatha Mushi alisema alipokea kwa masikitiko msiba wa mdogo wake kwa sababu alikuwa mtu mwelewa na msikivu katika jamii ambayo wamekulia.
Eviolatha alitoa wito kwa wanandoa kumshirikisha Mungu katika maisha yao na sio mwanadamu, hali itakayosaidia kutatua matatizo wanayopitia kwa kuwa neno la Mungu linasema kila mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke lazima atalamba mauti, hivyo hawana budi kukubaliana na neno hilo.
Naye, mdogo wa marehemu, Happy Mushi, alisema hadi sasa hawezi kuamini chochote hadi polisi itakapotoa majibu ya upelelezi .
Alisema Oktoba 9, mwaka huu, marehemu alimpigia simu na kumwambia anamshukuru Mungu, kwani ametoka kufanya kazi katika mazingira magumu, hivyo muda si mrefu anaweza kuhamia Tanzania, na kwamba yupo nchini kwa ajili ya kumalizia nyumba yake ambaye ipo Mbezi, Dar es Salaam.
Lakini cha kushangaza kabla ya wiki alisikia katika vyombo vya habari vikitangaza kaka yake amejiua mwenyewe pamoja na familia ya mke wake,î alisema.
Mwili wa marehemu ulisafirishwa jana kwenda kijijini kwao Ongoma Timbirini na unatarajiwa kuzikwa leo.
Wakati huo huo, Ufoo aliyelazwa Muhimbili hali yake imetengemaa na ameanza kutembea pamoja na kwamba daktari anayemhudumia anakataza watu kuingia kumtazama.
Ofisa wa Habari wa MNH, Aminiel Eliegaisha, alisema jana kuwa, Ufoo anaendelea vizuri na ameanza mazoezi ya kutembea, ingawa bado hawajaanza kuwaruhusu watu kwenda kumtaza kwa sababu ameshonwa sehemu nyingi na kwamba wanahofia kidonda kutokupona haraka.
Tukio hilo la mauaji lilitokea Oktoba 13, mwaka huu, eneo la Kimbamba nyumbani kwa wazazi wa Ufoo, ambapo alikwenda akiwa na mzazi mwenzake Anthery Mushi. Mushi alimuua mama wa Ufoo kwa kumpiga risasi zinazosadikika tano na kumjeruhi kabla ya kujiua mwenyewe.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru