Tuesday 8 October 2013

Bilal aagiza wezi wakamatwe


NA RODRICK MAKUNDI, HAI
MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Billal, ameagiza watu waliohusika na wizi wa fedha za kuwalipa fidia wananchi kwenye maeneo ilikopita miradi ya umeme wakamatwe na kuchukuliwa hatua.
Dk. Billal alitoa agizo hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, wakati akiwa kwenye ziara ya siku kuzindua miradi ya kupokea na kusambaza umeme.
Alisema watu hao wamefanya wizi wa sh. milioni 167, hivyo alisisitiza kwamba serikali haiwezi kuwavumilia, kwani wanazifanya nchi wahisani kukata tamaa ya kuisaidia Tanzania.
Makamu wa Rais, alisema moja ya vigezo vya wahisani walioonyesha nia ya kushirikiana na Tanzania kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ni usimamizi mzuri wa fedha, hivyo lazima serikali iendelee kulinda uaminifu huo.
Alisema nchi kama Japan ni wahisani wakubwa wa Tanzania katika kutekeleza miradi ya umeme kupitia misaada inayoendelea kuitoa kwa taifa hili.
Awali, Gama alisema kwenye utekelezaji wa mpango wa ulipaji fidia, wako baadhi ya watu waliolipwa fedha hizo, ambao hawakustahili kulipwa.
Hata hivyo, alisema licha ya dosari iliyojitokeza miradi inayoendelea kutekelezwa itaimarisha ukuaji wa uchumi wa wananchi kuongeza uwezo na uhakika wa upatikanaji wa umeme.
Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada, alitoa wito kwa Tanzania kuandaa mipango ya muda mrefu ya matumizi ya aina mbalimbali ya nishati zilizopo.
Alisema nishati ya joto ya ardhi ni sehemu mojawapo inayoweza kukidhi mahitaji ya ongezeko la matumizi ya umeme nchini.
Naye, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema miradi mitano ya kupokea na kusambaza umeme katika mkoa wa Kilimanjaro imetekelezwa kwa gharama ya sh. bilioni 44.
Aliitaja miradi iliyotekelezwa ni pamoja na Kiyungi, Lawate, Himo, KCMC na Makuyuni, na kuongeza kuwa ifikapo mwaka 2015, Tanzania itakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme unaotosheleza mahitaji na kiasi kingine kuuzwa nje ya nchi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru