Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushiriki, Mhandisi Christopher Chiza, amepewa siku 21 kuwasilisha taarifa kwa umma kueleza hatua zilizochukuliwa na wizara yake kuwakomboa wakulima wa korosho dhidi ya walanguzi.
Pia, ametakiwa kueleza sababu za kuyumba kwa bei ya korosho, kuchelewa kwa malipo pamoja na tozo nyingi walizowekewa wakulima wa korosho kunakosababisha na udhaifu na ukosefu wa maadili ya baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika.
Agizo hilo limetolewa na Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), baada ya kukutana na kujadili kwa kina masuala yote yanayohusu korosho na changamoto zinazowakabili wakulima wa zao hilo nchini.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda, aliwaeleza waandishi wa habari mjini hapa, jana kuwa, kuyumba kwa bei ya korosho pamoja na kuchelewa kwa malipo kumekuwa kukirudisha nyuma maendeleo na harakati za wakulima nchini katika kupambana na umasikini.
Alisema kamwe UVCCM haiwezi kuvumilia mambo yanavyokwenda katika korosho kwa sasa, na kwamba watahakikisha kero hiyo ambayo inawakabili wakulima wengi inapatiwa ufumbuzi na serikali kupitia watendaji waliopewa jukumu la kusimamia.
“Baraza linamtaka Mhandisi Chiza kufanya uamuzi wa dharura wa kushughulikia matatizo hayo ndani ya siku 21 na kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatua zilizochukuliwa ili kuwaokoa wakulima wa korosho na unyonyaji unaofanywa na walanguzi na pamoja wajanja wachache,’’ alisema Sixtus.
Pia, alisema Baraza Kuu limeiagiza serikali kuachana na mipango isiyotekelezeka, ikiwa ni pamoja na kodi ya laini ya simu za mkononi ambayo inatozwa sh. 1,000 kwa mwezi, kwani itakuwa na madhara makubwa iwapo itatekelezwa kwa kuwa waathirika watakuwa watu wa kipato cha chini.
Katika kikao chake kilichoketi juzi, Baraza hilo limemteua Paul Makonda kuwa Mkuu wa Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji, Zainab Athuman Katimba kuwa Mkuu wa Idara ya Organizesheni na Siasa na Omar Seleman kuwa Mkuu wa Idara ya Utawala, Uchumi na Fedha.
Tuesday, 29 October 2013
UVCCM yatoa siku 21 kwa Waziri Chiza
08:49
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru