Thursday 31 October 2013

Mfumo mbovu wa elimu wafumuliwa


NA SELINA WILSON
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imefuta mfumo wa zamani wa viwango vya upangaji wa alama za ufaulu kwa kidato cha sita na nne, ambapo kwa sasa hakutakuwa na daraja sifuri badala yake kutakuwa na daraja la tano.
Mfumo huo mpya ambao utaanza kutumika mwaka huu kwa kidato cha nne na mwakani kwa kidato cha sita pia watahiniwa wataanza kutumia alama za mitihani na kazi za mradi (project) kuanzia mtihani wa taifa wa kidato cha pili.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome aliwaambia hayo jana, waandishi wa habari kuhusu mabadiliko hayo  ambayo yanalenga kuimarisha mfumo wa elimu nchini na kuweka uwazi kwenye mitihani.
Alisema kuanzia mwaka huu mtihani wa taifa wa kidato cha nne utakuwa alama 60 na alama 40 zitapatikana katika mtihani wa taifa wa kidato cha pili, mitihani ya mitatu ya mihula ya kidato cha tatu na mazoezi ya vitendo.
Akifafanua katika alama hizo 40 za CA, Profesa Mchome alisema mtihani wa taifa wa kidato cha pili utakuwa na alama 15, matokeo ya mihula mitatu ya kidato cha tatu kila mmoja utakuwa na alama tano, mtihani wa majaribio wa kidato cha nne utakuwa na alama 10 na kazi za mradi itakuwa alama tano.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea ambao wanarudia mitihani, CA zao zitakazotumika ni zile zilizotoa matokeo ya mtihani wa awali na kwa watahiniwa waliopitia mfumo wa QT matokeo yao ya awali nayo yatatumika CA kwenye mtihani wa mwisho kuchangia alama 60.
Kuhusu viwango vya alama, Profesa Mchome, alisema kutakuwa na alama A, C, D, E na F yatakuwa kwenye kundi moja moja, lakini alama B itagawanywa kwenye makundi mawili kwenye alama B+ na B.
Profesa Mchome alisema mchanganuo wa alama na tafsiri yake utakuwa kama ifuatavyo: Alama A itakuwa na maana ya ufaulu uliojipambanua, B+ itakuwa ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana.
Alisema alama D itakuwa ni ufaulu wa wastani, E itakuwa ni ufaulu hafifu (Very Low Perfomance) na F ni ufaulu usioridhisha (Unsatisfactory perfomance).
Katika uchambuzi wa matokeo kulingana na alama hizo, alisema A itakuwa na pointi 26 na kwa alama 75 hadi 100, B+ itakuwa na pointi 15 kwa alama  alama 60 hadi 74, B itakuwa na pointi 10 kwa alama 50 hadi 59, C itakuwa na alama 40 hadi 49 na D itakuwa na alama 30 hadi 39 na zote zitakuwa na pointi 10.
Profesa Mchome alisema E itakuwa na alama 20 hadi 29 nayo itakuwa na pointi 10 na F itakuwa na pointi 20 na alama 0 hadi 20, kwa maana ya ufaulu usioridhisha.
Kuhusu madaraja, alisema kuanzia mwaka huu kwa kidato cha nne hakutakuwa na daraja sifuri na badala yake mfumo wa madaraja utaanzia na daraja la kwanza ambalo litakuwa na kundi la ufaulu uliojipambanua na ufaulu bora sana, daraja la pili litakulokuwa na kundi la ufaulu mzuri sana.
Alisema daraja la tatu litakuwa na kundi la ufaulu mzuri na ufaulu wa wastani, daraja la nne litakuwa na kundi la ufaulu hafifu na daraja la tano litakuwa na kundi la ufaulu usioridhisha.
Katika hatu nyingine, Profesa Mchome alisema wizara inatarajia kuanza kutumia muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (GPA) mwakani katika matokeo ya mitihani na kuondoa alama S katika mitihani ya kidato cha sita.
Alisema muundo huo mpya utatumika kwa mzunguko wa miaka minne kabla ya haujahuishwa tena ili kutoa muda wa kutosha kuona aina ya changamoto zinazojitokeza na jinsi ya kuzishughulikia.
“Aina hii ya muda itaruhusu vidato vinne vya elimu ya sekondari ya kawaida na nane ya elimu ya sekondari ya juu kupimwa,” alisema na kuongeza  kuwa uhuishaji wa masuala hayo ya mtihani unaweza ukafanyika iwapo matokeo ya kawaida ya uhuishaji wa mitaala, utahitaji pia eneo la mitihani liguswe na kuhuishwa.
Alisema kinachofanyika kwa sasa ni kuendelea kukusanya maoni ya wadau na kufanya maandalizi ili utaratibu huo wa GPA uanze mwakani.
Profesa Mchome alisema mabadiliko hayo ni mwendelezo wa mikakati ya wizara, na kwamba yapo mabadiliko ya mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya kufundishia na kujifunzia, vitabu na vifaa vingine muhimu katika elimu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru