Tuesday, 22 October 2013

Mjumbe wa NEC azikwa


Na Frank Kibiki, Njombe
MWENYEKITI wa CCM mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, ameongoza mamia ya waombolezaji wa mkoa wa Njombe katika maziko ya aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Wilaya ya Njombe mjini na Diwani wa Kata ya Njombe Mjini, Lupyana Fute.
Marehemu Fute, alifariki dunia juzi kutokana na shinikizo la damu, baada ya kupewa taarifa za chumba kimoja cha kuhifadhia vifaa vya ofisini kwake, kuungua moto.
Akitoa salamu za pole, Msambatavangu, alisema kifo cha Fute kimeacha pengo kubwa kwa Chama na serikali.
“Tulimjua Fute kama mpiganaji ndani ya CCM na serikali yake, hatuna la kusema zaidi ya kumuomba Mungu ampumzishe kwa amani, Amina,” alisema Msambatavangu.
Akitoa salamu kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Gerson Lwenge, alisema serikali imepoteza mtu muhimu na kwamba, kila mmoja atumie muda wake kumuombea ili apumzike kwa amani.
“Serikali imepoteza mtu muhimu, na wakazi wa mji wa Njombe wamempoteza diwani wao waliyemtegemea katika shughuli za maendeleo, wote tumuombee na kushirikiana na familia yake katika wakati huu mgumu,” alisema Lwenge.
Naye Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Njombe, Askofu Isaya Mengele, aliwataka wanasiasa kutumia harakati zao katika kuyaenzi yale yote ambayo kiongozi huyo alikuwa akiyafanya.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru