Tuesday, 8 October 2013

Ujenzi chuo Ihemi wapamba moto


NA FRANK KIBIKI, IRINGA

MAKATIBU wakuu wa vyama vitano vilivyopigania uhuru katika nchi za Kusini mwa Afrika, na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), wamefanya ziara katika eneo la Chuo cha Uongozi cha Vijana wa CCM Ihemi mkoani hapa.
Ziara hiyo ni mkakati wa kuanza ujenzi wa chuo hicho kwa  pamoja cha kisiasa.
Vyama hivyo ni  MPLA cha Angola, Frelimo cha Msumbuji, SWAPO Namibia, ZANU- PF Zimbabwe, ANC Afrika Kusini na CPC cha China na wenyeji Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza wakati akiwatembeza viongozi wa vyama hivyo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Itikadi na Uenzi, Nape Nnauye alisema lengo la ziara hiyo ni kutekeleza maagizo ya vikao vya vyama hivyo katika kuhakikisha ujenzi wa chuo hicho unaanza mara moja.
Nape alisema tayari zimetengwa hekta 1,830 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho cha kisiasa chenye lengo la kuwanoa makada wa vyama hivyo, ili viendelee kushika madaraka kwenye nchi zao na kuenzi fikra za waasisi wa vyama hivyo.
“Sababu za kuchagua eneo la Ihemi kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki cha kisiasa ni kuenzi historia ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini na Angola, ambao waliishi eneo la Kihesa-Mgagano, mkoani hapa kujiandaa kukomboa nchi zao,” alisema Nnauye.
Mbali na sababu hiyo, alisema eneo hilo lipo mbali na makazi ya watu, na kwamba limetulia, hivyo linafaa kuwa chuo cha kiitikadi kwa makada wa vyama hivyo.
Alifafanua kuwa, wamegawa eneo la Ihemi kwa makundi mawili, likiwemo lile ambalo vijana wa vyama hivyo watajenga chuo chao kwa ajili ya kujinoa ili baadaye waje kuwa viongozi bora.
“Chuo hicho kitahudumia vyama rafiki vilivyopigania uhuru katika nchi za Kusini mwa Afrika, na tumeanza mkakati mkubwa wa ujenzi ndio maana baada ya maazimio ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, leo tumekuja hapa tukiambatana na Balozi wa China,” alisena Nnauye
Pia, alisema chuo hicho kitatoa elimu ya  uongozi na kitasaidia katika masuala ya ujasiriamali ambayo yatawawezesha vijana kuweza  kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa.
Katibu Mkuu wa SWAPO nchini Namibia, Nangolo Mbumba alisema kuwa, wameridhishwa na eneo hilo la Ihemi, na kwamba litakisaidia chama chao katika kuendelea kuwapata viongozi walionolewa kiitikadi na kisiasa.
Mbumba ambaye pia aliwahi kuishi eneo la Kihesa - Mgagao, alisema Tanzania ina kila sababu ya kujivunia ujenzi wa chuo hicho, ikiwa ni njia ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alivisaidia vyama vyao kujikomboa kutoka kwa wanyonyaji.
Naye, Ofisa Habari wa Chama cha MPLA, alisema wana imani kwamba, ujenzi wa chuo hicho utaendelea kutunza kumbukumbu kwa vizazi vijavyo jinsi waasisi walivyoweza kupigania uhuru wan chi zao.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Uhusiano wa Afrika wa Kamati Kuu ya CPC, ambacho kinashiriki katika ujenzi wa chuo hicho, Zhong alisema serikali ya China  imekusudia kushirikiana na vyama hivyo katika kufufua  chuo  cha Ihemi kwa kufanya ukarabati mkubwa na kujenga majengo mapya.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha SWAPO, Jekero Tweya alisema baada ya kutembelea chuo hicho, makatibu wakuu watakutana kwa lengo la kuona namna gani wanaweza kuanza ujenzi huo mara moja.
Hivi karibuni, Balozi wa China,  Youqng alisema pamoja na majengo mengi, nchi hiyo imedhamiria kujenga hosteli za wageni na kusaidia kutunza baianuwai ya eneo hilo ambayo itakuwa kivutio cha wageni na sehemu ya utalii kwa watu watakaotembelea mkoani hapa.
Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Yahaya Msigwa alisema kuwa chuo hicho cha uongozi cha siasa cha Ihemi, kilikuwa maarufu wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere kutokana na kutoa mafunzo kwa vijana na kwamba kitakuwa msaada mkubwa kwa Chama baada ya kukamilika.
Aliongeza kuwa ujenzi na ukarabati wa chuo hicho, unarudisha hadhi yake kwa kupika viongozi vijana ambao, watapata uzoefu kutoka nchi za Kusini mwa Afrika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru