Tuesday 8 October 2013

JK ashtukia ahadi za kuchomekewa


SELINA WILSON NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA
RAIS Jakaya Kikwete ameagiza viongozi wa mkoa wa Pwani kumaliza tatizo la kiutendaji linalosababisha kuzorota kwa  utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Rufani ya Tumbi mjini hapa, hivyo kusababisha kero katika kituo cha afya Mkoani.
Tatizo hilo linasababisha wagonjwa kurundikana katika Kituo cha Afya Mkoani, huku Hospitali ya Tumbi ikibaki bila wagonjwa na badala kuhudumia wanaopata ajali katika barabara kuu za Morogoro na Chalinze/Segera.

Amesema hali hiyo inasababishwa na utata baina ya viongozi ambao wapo kwenye giza la madai kuwa Hospitali ya Tumbi ni ya Shirika la Elimu Kibaha (KEC), hivyo aliagiza kuanzia sasa washughulikie tatizo hilo na kutoa huduma kwa wananchi.
Rais Kikwete alisema hayo jana mjini hapa katika siku ya tano ya ziara yake mkoani Pwani, ambapo aliwashukia watendaji wa mkoa, wilaya na KEC kwamba ndio chanzo cha kuyumbisha juhudi za serikali za kuboresha huduma za afya.
Hatua hiyo ya Rais Kikwete ilitokana na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Sylvestry Koka kueleza ukweli wa tatizo la sekta ya afya, hususan wananchi kunyimwa huduma katika Hospitali ya Tumbi kwa madai ni hospitali ya rufani.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha msongamano mkubwa katika vituo vya afya, huku wagonjwa wengi, hususan wajawazito wakilala watatu kitanda kimoja na wengine chini.
Kutokana na hilo, Rais Kikwete aliwataka viongozi wote kuelekeza jitihada za kujenga hospitali ya wilaya, na kwamba kuwa hospitali ya mkoa ndio ile ya Tumbi na kwenye hilo hakuna mjadala, kwani shirika ni mali ya serikali.
‘’Niliwahi kusikia mnatembeza bakuli, mkatumia Mzee Ali Hassan Mwinyi, mliniomba mchango nikakataa kutoa na leo ndio nawaeleza sababu, kwamba serikali ina utaratibu wake na haiwezi kujenga hospitali ya mkoa kwa kutembeza bakuli,
“Hospitali za mkoa zinajengwa kwa fedha za serikali kuu, nyie viongozi mlijichanganya wenyewe kutokana na fikra kwamba tumbi ni hospitali ya Shirika la Elimu Kibaha, ndio maana mmeshindwa kupata fedha za kujenga hospitali ya mkoa,’’ alisema.
Aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanaweka nguvu zao katika kutatua tatizo la upungufu wa vifaa katika Hospitali ya Tumbi na kujenga hospitali ya wilaya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Awali, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Dk. Issa Kaniki alisema bado kuna changamoto kubwa katika Hospitali ya Tumbi, ambapo zinahitajika sh. bilioni 11 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upasuaji mkubwa na  mapokezi, hususan sehemu ya kuhudumia majeruhi wa ajali za barabarani.
Wakati huo huo, Rais Kikwete aliwashtukia watendaji wa  wilaya ya Kibaha kwa kumchomekea ahadi  ambazo hajazitoa wakati wa kampeni za uchaguzi, ambapo alisema kila alichoahidi anakijiua na zingine ni za ilani ambazo zina utaratibu wake.
“Hizi ahadi zingine jamani mnanichomekea si zangu, hivi kweli mimi niliahidi barabara ya lami Makofia/Mlandizi hadi Vikumburu Kisarawe na  Kwa Mathias/Msangani, hizo sikuahidi, lakini zipo kwenye Ilani ya Uchagauzi ya CCM, zina mipango yake,” alisema.
Katika ziara yake mjini hapa, Rais Kikwete aliweka jiwe la msingi ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa za kuua mazalia ya mbu kinachoendelea kujengwa katika mtaa wa Machinjioni, kilichojengwa na serikali ya Tanzania kwa kutumia teknolojia ya Cuba, ambacho ujenzi wake unagharimu sh. bilioni tano.
Alisema shabaha ya kujenga kiwanda hicho ni kutokomeza malaria na kuokoa maisha ya Watanzania na hilo litawezekana baada ya kukamilika kwa kiwanda hicho kitakachoanza kazi Desemba, mwaka huu.
Kabla ya kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara Mlandizi, Rais Kikwete aliweka jiwe la msingi la jengo la Halmashauri ya Mji Kibaha, ambapo katika awamu ya kwanza linagharimu sh. bilioni 5.2. ambapo kwa sasa vyumba 42 vimekamilika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru