Tuesday, 29 October 2013

Askofu Mkude atia neno Katiba Mpya


na mwandishi wetu
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Mhashamu Telesphory Mkude, amemsifia na kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuanzisha, kusimamia na kuongoza vizuri mchakato wa kutungwa kwa Katiba mpya nchini.
Pia, amewataka wananchi badala ya kukaa na kulalamika, wajitokeze kutoa maoni yao ili kuboresha mchakato huo utakao iwezesha Tanzania kupata Katiba nzuri itakayoiongoza kwa miaka mingine 50 ijayo.
Aidha, Askofu Mkude, amemwelezea Rais Kikwete kama kiongozi wa mfano ambaye anawajali wananchi na kushirikiana  nao katika kujitafutia maendeleo.
Aliyasema hayo katika sherehe za Jubilee ya miaka 100 ya Parokia ya Lugoba, iliyopo Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Sherehe hizo zilifanyika mwishoni mwa juma lililopita katika Kanisa la Msalaba Mtukuka.
Askofu Mkude, aliwaambia mamia ya waamini na wakazi waliojitokeza kuhudhuria sherehe hizo kuwa, katika eneo hilo, kuna shule ambayo Rais Kikwete alisoma mwanzoni mwa miaka ya 1960.
“Umefanya mengi sana wakati wa kipindi cha uongozi, lakini moja ya mambo hayo makubwa ni kuanzisha, kusimamia na kuongoza mageuzi makubwa ya kutungwa kwa Katiba mpya katika nchi yetu. “Tunakupa heko sana kwa kusimamia jambo hili ambalo litatuwezesha sote kupata Katiba inayotokana na ridhaa ya wananchi,” alisema.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria sherehe hizo ni Askofu Anthony Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga.
Akizungumzia nafasi ya wananchi katika mchakato huo, Askofu Mkude alisema: “Tuache kunung’unika. Tutoe maoni ya kuiboresha. Si viongozi wengi wanatoa nafasi kama hii duniani kwa wananchi wao kushiriki katika kujadili Katiba yao wenyewe. Kama asingependa, Rais Kikwete angeweza kubakia na Katiba ya sasa ambayo ni nzuri pia.”
Kuhusu suala la amani, alisema ni muhimu kwa Watanzania kumuunga mkono Rais Kikwete kwa kuilinda na kuitetea badala ya kuivuruga.
Hata hivyo, alisema wapo miongoni mwa Watanzania ambao pengine hawaelewi maana ya amani, wameamua kuanzisha harakati za kutaka kuisambaratisha.
Aliwaonya watu hao kuacha mara moja mchezo huo, kwani ni hatari kwa maisha yao nay a Watanzania wote.
Mbali na kusoma katika Shule ya Kati ya Lugoba kati ya mwaka 1962 na 1965 wakati huo ikiitwa ‘St. John Bosco’s Lugoba Middle School’ iliyokuwa inamilikiwa na Kanisa Katoliki, Rais Kikwete amekuwa akichangia maendeleo ya shule na Parokia hiyo ya Lugoba mara kwa mara.
Kabla ya kilele cha sherehe hizo, Rais Kikwete alizindua rasmi zahanati ya Kanisa ambayo aliifanyia ukarabati na aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa ukumbi ambao unajengwa na Parokia hiyo kwa gharama ya sh. milioni 200.
Parokia ya Lugoba ilianzishwa miaka 100 na Mapadri wa Cornel na Herman, kwa kushirikiana na wenyeji akiwemo mtawala wa eneo hilo wakati huo, Mzee Kinogile.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru