Tuesday 22 October 2013

Majambazi yakomba mamilioni ya mishahara


NA ANITA BOMA, IRINGA
WATU wanaodhaniwa kuwa majambazi, wamemvamia Meneja wa Kampuni ya SIETCO, Zhao Yang na kumpora zaidi ya sh. milioni 135, ambazo ni mishahara ya watumishi wa kampuni hiyo.
Mbali na fedha hizo, majambazi hayo pia yalipora simu tano na funguo za gari, kabla ya kutokomea kusikojulikana.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, alisema wamefanikiwa kuokoa sh. milioni 80 na msako mkali unaendelea.
Akizungumza mjini hapa jana, Kamanda Mungi alisema Zhao (23), ambaye ni meneja wa kampuni hiyo inayojenga barabara ya Iringa-Dodoma, alikuwa na wenzake katika gari wakisafirisha fedha hizo kwenda katika kambi ya kampuni hiyo iliyopo Mtera.
Alisema Zhao akiwa na wenzake hao ambao ni raia wa China, walichukua fedha hizo katika Benki ya CRDB, tawi la Iringa na kuanza safari.
Alisema walipofika eneo la Mlima Nyang’oro, walikuta lori likiwa limeziba  njia, hivyo kulazimika kusimama.
Ndipo ghafla walijitokeza vijana watano wakiwa na silaha na kuwapora.
“Walipojitokeza hao majambazi waliwataka wachina kuwapa mfuko wa fedha nao bila kubisha walifanya hivyo. Walitoboa magurumu ya gari kwa misumari kisha wakatoweka na funguo,’’ alisema.
Kamanda Mungi, alisema kufuatia tukio hilo, walianza msako mkali na usiku wa kuamkia jana, walipambana na majambazi hayo kwa kurushiana risasi ambapo yalidondosha mabegi mawili ya fedha pamoja na silaha aina ya Shortgun.
Pia, alisema jambazi mmoja alinaswa akiwa ndani ya daladala eneo la Itono, ambapo alikutwa na pochi na vifaa mbalimbali vya wachina hao.
Mpaka sasa anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru