Wednesday 9 October 2013

Dk. Salim awavaa mafisadi


Na Neema Mwangomo
WAZIRI Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim amesema vitendo vya rushwa, ufisadi na malumbano vinavyofanywa na baadhi ya viongozi nchini vinatokana na kushuka kwa maadili.
Dk. Salim aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, alipohojiwa kuhusiana na maadhimisho ya miaka 14 tangu kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema kushuka kwa maadili miongoni mwa jamii ni chanzo kikubwa cha baadhi viongozi kusahau wajibu wao wa kulijenga taifa lililoasisiwa na Mwalimu Nyerere, ambaye uongozi wake ulizingatia misingi ya maadili bila kuangalia dini, rangi wala kabila.
ìNi muhimu kufahamu na kuthamini mchango wa Mwalimu. Angefufuka leo, jambo lingelomshangaza na kumuudhi ni rushwa, ufisadi, udini, tofauti za kikabila na utaifa...
“Pia, angeshangazwa na maendeleo ya nchi kutokana na juhudi kubwa zinazofanyika katika kuhakikisha maendeleo yanakua,î alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Salim, baadhi ya viongozi nchini wamekuwa hawafuati misingi ya Baba wa Taifa na wengine kufikia hatua ya kulumbana kwa kutoleana maneno makali hata ndani ya Bunge, na kuonya kuwa hali hiyo isipodhibitiwa nchi itapotea.
Alisema anasikitishwa na vitendo hivyo, kwani demokrasia si fujo na Bunge ni mahali patakatifu, hivyo wabunge hawana budi kupaheshimu na
kulumbana kwa nguvu ya hoja na si vinginevyo.
Dk. Salim ambaye ni Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, aliwataka wanasiasa nchini kuondoa tofauti zao ili kupata katiba bora, kwani katiba itakayopatikana ni ya Watanzania wote.
Alisema ili katiba bora ipatikane kuna haja ya kuwepo kwa maridhiano kwa watu wote na si kuufanya mchakato huo kuwa wa kisiasa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru