Tuesday 1 October 2013

Walimu 529 wafutwa kazi


NA SELINA WILSON
WALIMU 529 wamefutwa kazi kwa sababu za utoro, katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2010 hadi Juni mwaka huu.
Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma, ilisema idadi hiyo ni kati ya walimu 669 waliokuwa wanakabiliwa na kesi za utoro wa kuanzia siku tano na kuendelea.
Mkuu wa Kitengo cha Maadili na Nidhamu, Christina Hape, alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam,wakati akijibu swali la mwandishi wa habari hii, kuhusu hatua zilizochukuliwa na tume hiyo dhidi ya walimu wanaotoroka katika vituo vya kazi.
Christina alisema tatizo la utoro ni kubwa, na kwamba limekuwa likishughulikiwa katika ngazi za halmashauri kwa utoro wa chini ya siku tano, lakini kuanzia siku tano na kuendelea, idara yake ndio inayoshughulikia.
Alisema hatua ya kuwatimua walimu hao imechukuliwa kwa mujibu wa kanuni ya 57 ya utumishi wa umma, ambayo inaitaja adhabu ya kufukuzwa kazi kwa mtumishi anayetoroka kituo cha kazi kuanzia siku tano.
Akifafanua kuhusu tatizo la utoro kwa mwaka, alisema mwaka 2010/11, tume ilipokea mashauri 260 ya walimu watoro, 2011/12 mashauri 152 na mwaka 2012/13 kulikuwa na mashauri 257, ambapo jumla ni 669.
Christina alisema katika mashauri hayo, 529 iliamriwa wafukuzwe na mashauri ya walimu 140  bado yanaendelea kufanyika kazi.
Alisema katika ngazi ya wilaya, walimu 1,128 walipewa adhabu mbalimbali kutokana na makosa ya utoro usiozidi siku tano.
Kuhusu kesi za walimu wanaojihusisha na mapenzi  na wanafunzi, Christina alisema, tume ilishughulikia walimu 84, ambapo mwaka 2008/09 walimu 40, 2009/10 walimu 20, mwaka 2010/11 walimu 17 na mwaka 2011/12 walimu 11, na kwamba baadhi yao wameonywa na wengine kufukuzwa kazi.
Hata hivyo, Mwanasheria wa Tume hiyo , Redemta Senga, alisema kumekuwa na changamoto kubwa katika kushughulikia mashauri hayo kutokana na kukosa ushahidi.
“Baadhi ya watuhumiwa wamekuwa wakishirikiana na walalamikaji kupoteza ushahidi, wakati mwingine wanafunzi kupewa vitisho au wazazi kumaliza kesi kienyeji na hivyo kukwamisha utoaji wa adhabu,” alisema na kuongeza kuwa wanasisitiza kesi za namna hiyo zifikishwe polisi.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma, Edwin Mikongoti, alisema  serikali imekasimu madaraka kwa wakuu wa shule na walimu wakuu kuhusu usimamizi wa utumishi wa walimu ili kuongeza ufanisi.
Mikongoti alisema tume ina dhamana  ya kuhakikisha waajiri, mamlaka za ajira na nidhamu zinatekeleza mamlaka waliyopewa ya usimamizi na uendeshaji wa rasilimali watu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi ili kuimarisha utawala bora na uwajibikaji.
Alisema wakuu wa vyuo vya ualimu, vyuo vya maendeleo ya jamii, wakuu wa shule na walimu wakuu wanatakiwa kuwajibika katika kuwaeliemisha walimu kuhusu utaratibu wa masuala ya ajira katika maeneo ya ajira na usajili.
Pia, watashughulikia makosa madogo ya kinidhamu na kutoa adhabu, na madaraka hayo yamekasimiwa kwa makosa ambayo kama yakithibitika adhabu zake kwa mujibu wa kanuni namba 118, ya utumishi wa umma ya 2003, itakuwa ni kusimamisha nyongeza ya mshahara, kufidia hasara na karipio.
Mwaka jana, serikali ilisajili walimu wapya 11,000, lakini kumekuwa na tatizo walimu kuripoti na kutoroka katika vituo vyao vya kazi, huku wengi wao wakikimbia vijijini na kusaka uhamisho kwenda mijini.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru