Tuesday, 22 October 2013

Katiba mpya Vyama vyawasilisha maoni yao serikalini


Na Mohammed Issa
VYAMA vya siasa nchini, vimewasilisha mapendekezo yao kwa serikali, ikiwa ni sehemu ya kuboresha muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.
Hatua hiyo inatokana na maelekezo waliyokubaliana na Rais Jakaya Kikwete, kufuatia baadhi kudai muswada huo ambao tayari umesainiwa, una upungufu.
Pia, vimewaomba Watanzania hususan wabunge, waunge mkono juhudi za vyama hivyo, na serikali wahakikishe mchakato wa kupata Katiba Mpya unakuwa shirikishi, utakaolinda maslahi ya taifa.
Vyama hivyo vimesema kuwa vinatambua na kupongeza juhudi za Rais Kikwete anazozifanya za kutaka mchakato wa Katiba unasonga mbele kwa kuhuisha wadau wote.
Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia, alisema hayo jijini Dar es Salaam jana kuwa, mapendekezo hayo waliwasilishwa serikalini jana na wanasubiri kufanyiwa kazi.
Alisema kutokana na umuhimu wa upatikanaji wa katiba mpya, vyama hivyo vinaamini kuwa mchakato huo unafanyika kwa kulenga maslahi ya nchi na wananchi na si vyama vya siasa ama kundi la watu.
Kwa mujibu wa Mbatia, Rais Kikwete alipokutana na viongozi wakuu wa vyama vya siasa hivi karibuni, waliazimia mambo mbalimbali kwa maslahi ya taifa.
Alisema miongoni mwa mambo hayo ni kwa vyama vya siasa kuandaa mapendekezo ya upungufu wa muswada huo na kupendekeza marekebisho maalumu ambayo walikubaliana kuwa wayawasilishe serikalini.
Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, alisema baada ya kuwasilisha mapendekezo hayo, serikali itaunda kamati maalumu na vyama vya siasa kupitia TCD, navyo vitaunda kamati yake.
Alisema zitakutana na kujadiliana kwa kina upungufu wa muswada huo na kukubaliana kwenye maeneo yanayohitaji marekebisho kwa lengo la kuufanya mchakato huo kuwa shirikishi.
Mbatia, alisema baadaye, serikali itaanda hati ya dharura ili sheria husika irejeshwe bungeni katika mkutano wa bunge utakaoanza Oktoba 29, mwaka huu, kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho.
Mkutano huo, ulihudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbord Silaa.
Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa, ambaye anaviwakilisha vyama visivyo na uwakilishi bungeni, Aizek Cheyo (UDP) na Mama Nasmia kutoka TLP.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru