Na Cecilia Jeremiah
SERIKALI imetoa wiki mbili ikiwataka walimu ambao hawajarejea katika vituo vyao vya kazi ambavyo wamepangiwa kurejea katika vituo hivyo, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Kassim Majaliwa alipozungumza na Uhuru, Dar es Salaam jana.
Alisema baadhi ya walimu ambao wameshindwa kuripoti katika vituo vyao vya kazi ni wale waliopangiwa katika shule za msingi na sekondari katika halmashauri za mikoa mbalimbali nchini.
Majaliwa alishangazwa kusikia kuwepo kwa vitendo vya baadhi ya walimu kutoripoti katika vituo vya kazi kwa ajili ya kwenda kufundisha katika shule walizopangiwa, huku wakijua ni kosa kisheria.
Alisema kuwa serikali imejitahidi kuwalipa posho pamoja na mishahara kwa ajili ya kwenda kufundisha katika shule walizopangiwa.
Pia, aliwapongeza madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumburi, Tanga kwa kuutaka uongozi wa halmashauri hiyo kuwachukulia hatua za kinidhamu walimu watano waliopangiwa kufundisha katika shule za msingi katika wilaya hiyo na kutoripoti na kisha kutoweka taika vituo vyao.
Inadaiwa kuwa walimu hao hawajaripoti katika shule hizo zaidi ya miaka mitatu hadi hivi sasa.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru