Wednesday 30 October 2013

Shehena ya pembe za ndovu yanaswa


Na Tamimu Adam - Jeshi la Polisi
WAKATI taifa likiwa kwenye mjadala mkali na kampeni ya kusaka majangili nchini, polisi imekamata pembe 90 za ndovu zenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni moja.
Habari za kuaminika zinasema kuwa, pembe hizo zilikamatwa jana zikiwa kwenye gari aina ya Toyota Carina, iliyokuwa ikitokea Tunduru kwenda Masasi.
Hata hivyo, baada ya kunaswa, watuhumiwa walijaribu kumshawishi askari kumpa kiasi cha sh. milioni tatu ili aweze kuwaachia, jambo ambalo hakulifiaki, ndipo waliporuka kwenye gari na kukimbia. Pembe 90 ni sawa na tembo 45, ambao watakuwa wameuawa kwenye hifadhi za Taifa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen, alisema gari hiyo lilikamatwa katika Kata ya Maendeleo, baada ya polisi waliokuwa doria kuitilia shaka.
Alisema baada ya kuitilia shaka walimwamuru dereva kusimama na kuanza kufanya ukaguzi, ambapo kabla walimtaka kuonyesha leseni yake, ambayo hata hivyo hakuwa nayo.
Kutokana na hatua hiyo, askaru polisi hao waliamua kuchukua hatua zaidi ya kulikagua gari hilo, ndipo walipokuta shehena ya pembe hizo zikiwa zimehifadhiwa kwenye mifuko.
ìWatuhumiwwa hawa walijaribu kutaka kumuhonga askari aliyewakamata, lakini alikataa ushawishi huo na kuwafikisha kituoni. Huu ndio uzalendo na uadilifu,” alisema Kamanda Zelothe.
Alisema polisi inalishikilia gari hilo kwa hatua zaidi, huku wahusika wakiendelea kusakwa ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Katika ukaguzi huo, gari hilo lilikutwa na vitu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na simu ya kiganjani, mizani na nyaraka mbalimbali za benki.
Hata hivyo, taarifa za awali zinasema kuwa dereva wa gari hilo amebainika kuwa Oliver Lucas mkazi wa Masasi, huku mwenzake akiwa bado hajatambulika.
Pia, Kamanda Zelothe alisema kuwa, kigogo mwenye mzigo huo ametambuliwa kwa jina la Hassan Koko maarufu kama Twalib Nyoni.
Mapema juzi, mvutano mkali uliibuka bungeni kutokana na Kangi Lugola (Mwibara - CCM), kuibana serikali akitaka iwataje vigogo wanaohusika na ujangili.
Katika majadiliano hayo bungeni, ilielezwa kuna taarifa kuwa baadhi ya mawaziri, wabunge na maofisa wa vyombo vya usalama nchini, wanadaiwa kuhusika kwenye vitendo vya ujangili wa wanyama, hususan tembo na faru, ambao kwa sasa wapo kwenye hatari ya kutoweka.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru