Na Mohammed Issa
UMOJA wa Mataifa, umeipongeza serikali ya Tanzania kutokana na mchango wake kwenye jumuia za kimataifa.
Pia, umesema Tanzania imekuwa ikitoa ushirikiano mkubwa kwa umoja huo hapa nchini, na kwamba umekuwa ukifanya kazi zake bila ya usumbufu.
Pongezi hizo zilitolewa jana mjini Dar es Salaam na Mratibu wa Shughuli za Umoja huo nchini, Alberic Kacou alipokuwa akizungumzia maadhimisho ya miaka 68 ya UN.
Alisema serikali ya Tanzania inayoongoza na Rais Jakaya Kikwete imekuwa na mchango mkubwa katika jumuia ya kimataifa, hususan kwenye masuala ya ulinzi wa amani.
Kacou alisema maadhimisho hayo yataanza na wiki moja kabla ambayo ilianza jana na kilele chake kitafanyika Oktoba 24, mwaka huu, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe atakuwa mgeni rasmi.
Alisema shughuli mbalimbali zinatarajiwa kufanyika katika wiki ya UN, ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa mjadala wa wazi utakaofanyika Oktoba 22, mwaka huu, katika ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajabu Gamaha alisema siku ya Umoja wa Mataifa itaadhimishwa katika viwanja vya Karimjee mjini Dar es Salaam, ambapo Waziri Membe atapandisha bendera ya UN.
Alisema wananchi wanaombwa kuhudhuria mjadala wa wazi utakaofanyika Jumanne ijayo katika ukumbi huo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru