NA STEPHEN BALIGEYA, DODOMA
WABUNGE wamewajia juu mawaziri watoro kwa kueleza kuwa wanachangia kuzorota kwa mipango ya serikali, kwa kukosekana kwao kusikiliza maoni na ushauri unaotolewa na wabunge.
Hayo yalielezwa bungeni jana na wabunge mbalimbali walipokuwa wakichangia Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka 2014/2015, ambapo hadi inafika saa 12.08, walikuwemo mawaziri kamili saba tu kati ya 29.
Kafulila alisema kitendo hicho husababisha serikali kushindwa kusimamia utekelezaji wa mipango yake kwa kuwa, watu wanaotakiwa kufuatilia utekelezaji huo, hawako makini.
Vilevile, James Mbatia (Kuteuliwa), alisema kitendo kinachofanywa na mawaziri hakikubaliki na kinaonyesha jinsi ambavyo uwajibikaji na umakini haupo katika kusimamia shughuli za serikali.
Mbatia ambaye wakati akichangia kulikuwa na wabunge kamili wanne kabla ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kuingia, alisema hali hiyo imechangia mambo mengi yanayofanywa na serikali kuchukuliwa yale ya miaka ya nyuma na kurudishwa kila mwaka, kwa kuwa watendaji wa serikali hawako makini kusikiliza maoni ya wabunge.
Aidha, Modestus Kilufi (Mbarali - CCM), alisema tabia ya mawaziri kutohudhuria vikao vya bunge kunachangia kutoratibu na kusikiliza maoni ya wabunge, hivyo ushauri mwingi ungeoweza kusaidia kuboresha mipango ya maendeleo kutofanikiwa.
ìKwa nini mawaziri kama wana safari zao wasiwe wanazipanga wakati ambao usio wa Bunge, kwa nini kila bunge linapofika ndipo wanakuwa na safari nyingi?î alihoji Kilufi.
Katika kutoa ufafanuzi wa utoro wa wabunge, Waziri wa Nchi, Ofsi ya Rais asiye na Wizara Maalum, Profesa Mark Mwandosya, kwa niaba ya waziri Mkuu, alisema serikali inachukua maoni yote yanayotolewa na wabunge hata kama mawaziri hawapo bungeni.
ìSerikali inafanya kazi zake kwa taarifa na kila kitu kinachozungumzwa humu hata kama hakuna mawaziri kinachukuliwa na hata sisi wachache tuliopo tunachukua na kuwapelekea mawaziri husika kwa ajili ya kujibu hoja zenu.
Kwa hiyo, naomba wabunge muelewe kuwa maoni na ushauri wenu unachukuliwa, na humu kuna watendaji wengine wa serikali wanachukua maoni hayo, na pia hata makatibu wakuu hawapo hapa, lakini katika ofisi zao kuna televisheni na hivyo wanasikiliza, alieleza.
Katika siku ya kwanza ya kikao cha bunge la mkutano wa 13 ulioanza Jumanne, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliwataka mawaziri kuhudhuria katika majadiliano yanayofanywa na wabunge kwa kueleza kuwa mpango huo sio wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira, bali ni wa serikali nzima.
Nawaomba msije mkaacha kuja kusikiliza maoni na ushauri wa wabunge kwa kufikiri kuwa mpango huu ni wa Wasira, bali mawaziri wote mnahusika na hivyo mnatakiwa kuja kusikiliza na kila mmoja atajibu sehemu yake anayoguswa,î alieleza Makinda.
Lakini pamoja na ushauri huo wa spika katika kikao cha Jumanne wiki hii, mahudhurio ya mawaziri yamekuwa hafifu kiasi cha wabunge kuona kuwa mipango mingi ya serikali inashindwa kufanikiwa kwa sababu watendaji wake wanakosa kusikiliza ushauri wa wabunge.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru