Saturday 2 November 2013

CCM yampongeza Dk. Sheni kwa kutimiza miaka mitatu


Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar, Vuai Ali Vuai, amempongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni kwa kutimiza miaka mitatu tangu kuchaguliwa kwake.
Vuai alitoa pongezi hizo katika kikao kilichowahusisha watendaji wa Chama wa mikoa na wilaya za Unguja kilichofanyika jana katika Ofisi Kuu ya CCM, Zanzibar.
Alisema ndani ya kipindi hicho, Dk. Sheni ameweza kusimamia kwa umakini na uadilifu utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2010 -2015 na kusambaza maendeleo mijini na vijijini,  Unguja na Pemba kwa maslahi ya wananchi.
Vuai alisema utekelezaji wa ilani ya CCM unapaswa kwenda na ufanyaji kazi wa watendaji wa Chama kwa umakini na uadilifu mkubwa.
“Kila mtendaji kwa nafasi yake anapaswa kujituma katika kutekeleza majukumu aliyokabidhiwa na Chama na kutumia muda mwingi kutekeleza shughuli za Chama kwa uaminifu na uadilifu mkubwa ili kuleta maendeleo,”alisema.
Aliongeza kuwa wakati umefika wa kuleta mabadiliko na mafanikio mazuri ndani ya Chama na hilo litafikiwa iwapo watendaji hao watakuwa tayari kutekeleza shughuli za Chama kwa uadilifu na uaminifu kwa kusukumwa na mshikamano.
Naibu Katibu Mkuu huyo, alisema CCM ndio Chama pekee kinachoelewa shida zinazowakabili wananchi iwe mijini na vijijini, ambapo serikali zake zimekuwa mstari wa mbele kuyatolea majibu na kuzipatia utatuzi shida za wananchi.
Hivyo, aliwaagiza viongozi wa Chama kujipanga vizuri na kubuni mbinu na mikakati madhubuti itakayosaidia kufanikisha shughuli za Chama na Serikali.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru