Thursday 26 September 2013

Warioba: Katiba mpya haitaletwa kwa vurugu


Rabia Bakari na Mohammed Issa

TUME ya Mabadiliko ya Katiba, imeonya kauli na vitendo vya wanasiasa vinavyoendelea kuhusu mchakato wa kupata katiba mpya vinaweza kusababisha madhara na kuligawa taifa vipande.
Pia, imesema kuwa Katiba haiwezi kupatikana kwa maneno ya majukwaani, maandamano au vikundi kuzunguka nchi nzima na kwamba, msingi imara ni kutumia busara ya mazungumzo na maridhiano.
Mbali na hilo, imetahadharisha iwapo Katiba mpya ambayo mchakato wake unaendelea kwa sasa nchini itapatikana kwa mapambano, basi  hakutokuwa na umoja wala mshikamano wa kitaifa miongoni mwa Watanzania.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo alisema baadhi ya wanasiasa wanaingilia mchakato huo kwa manufaa binafsi na ndio sababu kelele haziishi kwenye majukwaa.
Vyama vitatu vya upinzani kwa sasa vipo kwenye kile kinachodai kufanya ziara nchi nzima kupinga Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa madai kuna vipengele vimechomekewa.
Wabunge wa vyama hivyo wakiongozwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, walisusia kikao cha Bunge kupitisha muswada huo, ambapo baadaye ilibainika kuwa mambo waliyotarajia kuyapenyeza hayakufanikiwa.
Pia, taarifa zinaeleza vyama hivyo vimekuwa kwenye mikakati kamambe ya kuhakikisha vinavuruga mchakato huo kwa maslahi yao binafsi, huku baadhi ya wafadhili wakiwa nyuma.
"Vyama vingi vya siasa vimejitazama vyenyewe, nia yetu ni kupata katiba ya wananchi wote... hatuko kwenye mashindano wala misuguano.
"Tunajenga, hatuko kwa ajili ya kubomoa... tunahitaji katiba itakayoheshimika na Watanzania wote na itakayokuwa chachu ya maendeleo," alisema Jaji Warioba na kuongeza kuwa.
"Kinachofanywa sasa na baadhi ya wanasiasa kinaweza kuleta madhara makubwa na kuwagawa Watanzania, hivyo kuiweka nchi katika wakati mgumu.
Jaji Warioba alisema kama kuna sehemu ambayo  wanasiasa wanadhani wametofautiana ni vyema kutafakari kwa pamoja kwa kukaa chini kwa lengo la kutafuta ufumbuzi na si kutumia majukwaa, jambo ambalo ni hatari na haliwezi kuwa na tija.
Alisema Katiba inayotafutwa ni ya Watanzania na sio kwa ajili ya vikundi vya watu, na kwamba umefika wakati kwa Watanzania kuungana na kutokubali kuyumbishwa.
Jaji Warioba alisema katiba itapatikana kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria na si maneno ya majukwaani.
Alisema tume hiyo sio msimamizi wa sheria, na kwamba inafanya kazi kwa kufuata taratibu za kisheria, zilizopitishwa na Bunge wakati wanakabidhiwa jukumu hilo.
Aliongeza kuwa baadhi ya vyama vya siasa wakati wa kupitia maoni ya kuboresha rasimu havikufuata utaratibu uliowekwa na vilitumia mihadhara kunadi matakwa yao.
Alisema wajumbe wa tume hiyo, walipata wakati mgumu na wengine walivurugwa kiakili kutokana na matamshi ya viongozi wa kisiasa walioamua kuvuruga utaratibu wa kukusanya mapendekezo ya rasimu.
Jaji Warioba alisema tume iliruhusu taasisi, asasi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana kuunda na kuendesha Mabaraza ya Katiba kwa lengo la kujadili na kuitolea maoni Rasimu ya Katiba Mpya.
Hata hivyo, alisema baadhi ya vyama vya siasa viliingilia uhuru wa wajumbe katika kutoa maoni na kuna maeneo mengine wajumbe wa mabaraza walifundishwa mambo ya kuzungumza.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, katika baadhi ya mikutano, wajumbe wa mabaraza waliwajadili wawakilishi kutoka tume, badala ya kuijadili rasimu ya katiba iliyotolewa.
Alisema pamoja na changamoto hizo, tume imetekeleza majukumu yake kwa kiasi kikubwa na hivi sasa wanachambua maoni, ili yaingie kwenye rasimu ya pili, ambayo itawasilishwa kwenye Bunge la Katiba.
Jaji Warioba alitumia fursa hiyo kukanusha taarifa kuwa kuna wajumbe wa Tume wamejiuzulu, ambapo alisema wajumbe wote wanaendelea na kazi waliyopewa na kwamba, hakuna aliyetishia kujiuzulu kama ilivyodaiwa.







Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru