Tuesday 9 July 2013

Dk. Magufuli akagua ujenzi barabara Dar


NA MOHAMMED ISSA
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema wanaokwamisha ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi wachukuliwe hatua.
Pia, amemuagiza mkandarasi anayejenga barabara ya Kigogo-Jangwani, kufanyakazi usiku na mchana ili ikamilike haraka.
Amemtaka asizivunje nyumba zenye kesi mahakamani, lakini maeneo mengine yote yawekewe lami, ili ianze kutumika.
Dk. Magufuli aliyasema hayo jana alipofanyaziara ya kutembelea miradi ya ujenzi wa barabara na daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Alisema ujenzi wa barabara ya Jangwani umechukua muda mrefu kutokana na baadhi ya wamiliki wa nyumba kuweka pingamizi mahakamani, wakidai kulipwa fidia kidogo.
Dk. Magufuli, alimuagiza mkandarasi anayejenga barabara hiyo, kufanyakazi usiku na mchana na kuhakikisha inakamilika katika kipindi kifupi.
“Ujenzi wa barabara uendelee kwa kasi na pale kwenye nyumba zilizowekewe pingamizi jengeni kwa kuzizunguka bila ya kuzivunja.
“Lengo la serikali ni kuhakikisha inajenga miundombinu mizuri na kupunguza foleni katika jiji la Dar es Salaam,” alisema.
Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 2.6, ulianza 2009 na ulitakiwa kukamilika mwishoni mwa 2010.
Hata hivyo, barabara hiyo imeshindwa kukamilika kwa wakati, baada ya wamiliki wa nyumba sita ambao wameshalipwa fidia kufungua kesi mahakamani, wakipinga fedha walizolipwa kuwa ni ndogo na kutaka waongezewe.
Ujenzi wa barabara hiyo mpaka kukamilika, utagharimu sh. bilioni 7.6 na sh. bilioni 3.8 zilitumika kuwalipa fidia wananchi waliopitiwa na mradi huo.
Dk. Magufuli alimuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kufungua kesi mahakamani dhidi ya wananchi hao kutokana na kuchukua fedha za serikali na wameshindwa kuondoka.
“Mtendaji Mkuu, unahaki ya kushitakiwa na kushitaki...basi na wewe wafungulie kesi hao watu sita waliochukua fedha za umma, lakini wameshindwa kuondoka.
“Haiwezekani watu wachache wale fedha za serikali bure na kama utashinda kesi basi gharama zote watalipa wao,” alisema.
Akikagua ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka katika eneo la Magomeni, Jangwani na Kivukoni, Dk. Magufuli aliuagiza uongozi wa mkoa kuwachukulia hatua kali wanaokwamisha mradi huo.
Alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo, ambaye alidai baadhi ya wanaokwamisha mradi huo ni wafanyabiashara wanaopanga biashara zao kando ya barabara.
Dk. Magufuli, alisema mtu yeyote atakayekwamisha ujenzi wa mradi huo achukuliwe hatua za kisheria haraka iwezekanavyo.
Mradi huo utagharimu sh. bilioni 288 na utakuwa na vituo 27 na vikubwa vitano na ndio mkubwa katika jiji la Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadiki, alisema mkoa umeanza kuchukua hatua kukabiliana na changamoto hizo.
Alisema amewaagiza Polisi kuwafikisha mahakamani mara moja waliofanyavurugu juzi eneo la Manzese na kusababisha uharibifu wa vifaa vya ujenzi wa mradi huo.
Akiwa katika barabara ya Kamata- Bendera tatu, Dk. Magufuli, aliwataka wananchi waliolipwa fidia kwa ajili ya kupisha ujenzi wa barabara hiyo kuondoka mara moja.
Alisema wote waliolipwa fidia wanatakiwa kuhama ifikapo Julai 19, mwaka huu, saa 12.00 asubuhi na siku hiyo, nyumba zote zinatakiwa zivunjwe.
Waziri huyo, alisema serikali ilitumia sh. bilioni 6.1 kwa ajili ya kuwalipa fidia na kwamba, itajengwa ya njia nne.
Akiwa katika daraja la Kigamboni, Dk. Magufuli, alimtaka mkandarasi anayejenga daraja hilo, kuhakikisha linamalizika kwa muda uliopangwa.
Alimtaka kuanzia sasa kufanyakazi usiku na mchana na lijengwa kwa ubora na viwango vinavyotakiwa.
Dk. Magufuli, alisema watu 113 wamefanyiwa tathimini na wamelipwa sh. bilioni 11.7, ambapo wanane wamekataa kulipwa.
Alisema mradi wa daraja hilo hadi kukamilika, utagharimu sh. bilioni 214 na aliwataka wananchi waliogoma kuchukua fidia kuchukua haraka kabla ya serikali haijafanya uamuzi.
“Daraja hili liliwekwa jiwe la msingi na Rais Jakaya Kikwete, hivyo tunataka aje alifunguwe mwenyewe,” alisema.
Kwa upande wake, Mhandisi Karimu Mataka, kutoka Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), alisema ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 47 na aliahidi kumalilizika kwa muda uliopangwa.
Akiwa katika barabara ya Davis Corner-Yombo, Dk. Magufuli alisema tathimini iliyofanywa isiongezwe tena.
Aliwataka wananchi kuondoa dhana kuwa kila panapojengwa mradi wa barabara watalipwa, kwani baadhi yao wanajenga katika hifadhi ya barabara.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, aliwataka wananchi kushirikiana na serikali inapotekeleza miradi ya maendeleo.
Pia, Waziri huyo alitembelea daraja la Salender ambapo alimuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kulifanyia upanuzi.
Alisema upande wa kushoto mwa daraja hilo magari madogo na pikipiki yaruhusiwe kupita ili kupunguza msongamano.
Dk. Magufuli, alimtaka mtendaji huyo, kujenga daraja lingine la muda ili magari yaweze kupita. Waziri huyo alitembelea pia ujenzi wa barabara eneo la Morocco na Lugalo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru