Friday 5 July 2013

Ushahidi kesi ya EPA wafungwa



NA FURAHA OMARY
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamua kufunga ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi ya EPA, inayowakabili Johnson Lukaza na nduguye, baada ya kukataa ombi la kuiahirisha.
Uamuzi huo ulitolewa jana baada ya jopo la mahakimu watatu, likiongozwa na Gabriel Mirumbe, kukubali hoja za wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa, aliyepinga kuahirishwa kwa kesi hiyo. Mahakimu wengine ni Edson Mkasimongwa na Pamela Mizengo.
Johnson na Mwesiga Lukaza, wanakabiliwa na kesi ya wizi wa sh. bilioni sita katika Akaunti ya Madeni ya Malipo ya Nje (EPA), mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Awali, Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro, alidai kesi hiyo ilipangwa kuendelea kusikilizwa lakini hawapo tayari kwa kuwa hakuna shahidi, hivyo aliomba iahirishwe kwa wiki moja.
Mgongolwa alipinga ombi hilo akidai mahakama ilishawahi kutoa uamuzi kuhusu maombi kama hayo na kusema inaahirishwa kwa mara ya mwisho.
Alidai hakuna sababu za msingi za kuahirisha kesi hiyo, hivyo kuomba hatua stahili zichukuliwe kwa kuamuru ushahidi wa upande wa Jamhuri ufungwe.
Kimaro alidai si kwamba hawana mashahidi, hivyo aliomba apewe wiki moja.
Mkasimongwa akisoma uamuzi wa jopo hilo, alisema hawawezi kuahirisha kesi hiyo kwa sababu imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara na kwamba, mahakama ilishatoa amri ya kuahirishwa kwa mara ya mwisho.
“Hatujaelezwa na wakili wa serikali kwa nini tuondoke kwenye amri ya kwanza, alichokisema hana mashahidi leo waliofika mahakamani anaomba apewe wiki moja.
“Kesi imekuwa ikiahirishwa kwa sababu za kukosekana kwa mashahidi. Kwa mara kadhaa imekuwa haisikilizwi. Tangu Novemba 27, mwaka jana hadi sasa ni miezi kama minane haijasikilizwa,” alisema.
Alisema vikwazo vya kujirudia vya kuahirishwa kwa kesi haviwapi nafasi ya kusikiliza shauri hilo haraka, hivyo haitaonyesha haki na haitakuwa sahihi kuvumilia.
Alipopewa nafasi ya kuzungumza, Kimaro alidai hana cha kusema na kwamba, wanatarajia kukata rufani dhidi ya uamuzi huo.
Kesi hiyo itatajwa Julai 11, mwaka huu, kutoa uamuzi iwapo washitakiwa wana kesi ya kujibu au la.



Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru