NA ANGELA SEBASTIAN, BUKOBA
MAJAMBAZI 10 yakiwa na silaha za kivita, yameteka mabasi mawili, kumpora askari polisi bunduki na kuiba mali za abiria.
Tukio hilo lilitokea jana saa 2.30 asubuhi katika eneo la Kasindaga, ndani ya Pori la Akiba la Biharamulo, mkoani Kagera.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Philip Kalangi, alisema majambazi hayo yakiwa na bunduki sita aina ya SMG na mbili aina ya LMG yaliteka mabasi hayo.
Alisema mabasi yaliyotekwa ni la Kampuni ya RS, lenye namba ya usajili T 495 AGT, lililokuwa likitoka Bukoba kwenda Dar es Salaam na NBS, lenye namba T 644 BUR, lililokiwa likitoka Bukoba kwenda Arusha.
Kamanda Kalangi alisema majambazi hayo yaliteka mabasi hayo baada ya kuwaweka chini ya ulinzi abiria na polisi wanne waliokuwa wakiyasindikiza.
Alisema majambazi hayo yaliwaamuru abiria kushuka ndani ya basi na kutoa kila walichokuwa nacho, zikiwemo simu na fedha taslimu.
Baada ya kutoa mali hizo, majambazi hayo yaliwaamuru abiria kulala kifudifudi.
Alisema abiria na polisi walitii amri hiyo, ambapo baadaye basi la Kampuni ya Mohamed Trans lililokuwa likitoka Bukoba kwenda Dar es Salaam, lilipita likiwa na askari, ndipo walipobaini wenzao wametekwa.
Kalangi alisema askari huyo alishuka ndani ya basi na kuanza kupambana na majambazi hayo, hivyo basi hilo kupata nafasi ya kuondoka.
Alisema askari huyo alizidiwa nguvu na majambazi hayo, ambayo yalimnyang’anya bunduki aina ya SMG, yenye namba ya usajili 14302551.
Kamanda alisema katika tukio hilo, Fredrick Rugaihura (47), mkazi wa Bukoba, aliyekuwa anakwenda Dar es Salaam, alibishana na majambazi hayo, hivyo yalimjeruhi kwa risasi shingoni.
Alisema Rugaihura amelazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Biharamulo kwa matibabu na kwamba, abiria wengine waliendelea na safari.
Kamanda alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linaendelea na msako ili kuyanasa majambazi hayo.
Alisema abiria walipohojiwa walisema majambazi hayo yalikuwa yakitumia lugha ya nchi za jirani. Thamani ya mali iliyoporwa bado haijajulikana.
Monday, 15 July 2013
Ujambazi wa kutisha
09:17
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru