Wednesday, 3 July 2013

Wafanyakazi 49 watimuliwa TANESCO


NA SELINA WILSON
WAFANYAKAZI 49 wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wamefukuzwa kazi kati ya Juni mwaka jana na mwaka huu, kutokana na kujihusisha na vitendo vya rushwa na wizi.
Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO, Injinia Felischemi Mramba, alisema hayo jana wakati akizungumzia hatua zinazochukuliwa katika kulisafisha shirika hilo, kwenye kongamano la wadau wa nishati na gesi.
Mramba, alisema watumishi hao ni kutoka kada mbalimbali wakiwemo mameneja  wa vitengo, mafundi na wataalamu mbalimbali.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema bado wanaendelea kuisafisha TANESCO na wananchi wenye kero au jambo linalohusiana na vitendo hivyo watoe taarifa ili hatua zichukuliwe.
Alisema hivi karibuni, walimsimamisha mfanyakazi wa shirika hilo baada ya kuzembea kushughulikia taarifa ya dharura ya kukatika umeme kwa siku saba.
Mramba alisema mlalamikaji alimpigia simu kutoa taarifa na hatua zikachukuliwa mara moja.
“Kwa TANESCO hakuna siri katika uwajibikaji, tulisaini mikataba ya utendaji bora na mameneja wa mikoa ili kuhakikisha wanatoa huduma stahiki, atakayezembea anachukuliwa hatua,” alisema Mramba.
Alisema mikataba hiyo walisaini mwaka 2007 na tangu kipindi hicho, kumekuwa na ongezeko kubwa la wateja wanaounganishiwa umeme.
Idadi hiyo imeongezeka kutoka wateja 36,000 hadi kufikia 94,000 mwaka jana.
Mramba alisema mambo waliyokubaliana ni utendaji bora, usimamizi na uaminifu wa wafanyakazi, hivyo inapotokea uzembe, hatua zinachukuliwa mara moja.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru