na waandishi wetu
RAIS Jakaya Kikwete amewashukuru wananchi kwa kushiriki kikamilifu na kufanikisha kwa kiwango cha juu matukio ya kitaifa, ikiwemo ziara ya siku mbili ya Rais Barack Obama wa Marekani.
Obama, mkewe Michelle na watoto wao Malia na Sasha walitua nchini Jumatatu wiki hii wakitoka Afrika Kusini na waliondoka juzi.
Matukio mengine yaliyofanyika kwa mafanikio kutokana na mchango wa wananchi ni Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote na Mkutano wa Wake wa Marais wa Afrika uliomalizika jana, jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa wageni maarufu walioshiriki mkutano huo ni Rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush na mkewe Laura. Pia ulihudhuriwa na wake wa marais wa Afrika Kusini, Ethiopia, Msumbiji, Ghana, Sierra Leone na Uganda.
Rais Kikwete pia amewashukuru viongozi na wasimamizi wa matukio na shughuli hizo, kwa kutoa uongozi thabiti ambao umewezesha mambo kumalizika vizuri na malengo yaliyokusudiwa kufikiwa.
Amevishukuru vyombo vya habari nchini kwa mchango mkubwa wa kutoa habari na kuwaelimisha wananchi kabla, wakati na baada ya matukio yenyewe.
Katika shukrani hizo, Rais Kikwete pia amezishukuru taasisi na vyombo vyote vya serikali, vikiwamo vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi bila kuchoka ili kufanikisha shughuli hizo.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wananchi wote, hususan wakazi wa Dar es Salaam, kwa mchango wenu mkubwa katika kufanikisha matukio haya muhimu ya kitaifa.
“Kwa pamoja tumeonyesha ukarimu wetu wa jadi kwa viongozi na wageni ambao wameshiriki katika matukio hayo,” alisema.
Aliongeza: “Tumeonyesha uvumilivu na utulivu mkubwa wakati wote wa matukio hayo. Natambua mazingira yanayojengeka tunapokuwa na ugeni mkubwa wa nje, lakini bado tumeonyesha ukomavu wa hali ya juu kama taifa.
“Nawashukuru ninyi wananchi kwa kufanikisha yote haya kwa sababu bila ushiriki wenu pengine matokeo ya shughuli hizo yangekuwa tofauti. Najivunia ushiriki wenu katika shughuli zote hizi za kitaifa. Mmeijengea nchi heshima kubwa.”
WASOMI WAMPONGEZA
Katika hatua nyingine, baadhi ya wasomi wamempongeza Rais Kikwete kwa jitihada za kuhakikisha diplomasia ya uchumi inakua.
Wamesema ziara za marais Xi Jinping wa China na Obama wa Marekani, zimemfanya Rais Kikwete kuiweka Tanzania katika alama ya kimataifa.
Kwa mujibu wa wasomi, ujio wa viongozi hao umefanyika wakati muafaka kwa Watanzania na kwamba, serikali imetenga maeneo maalumu ya ushirikiano wa kidiplomasia ili kuharakisha maendeleo.
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema Rais Kikwete anastahili pongezi, kwani ameonyesha uimara mkubwa katika diplomasia ya kimataifa.
“Tuipongeze serikali na Rais Kikwete kwa kuiweka Tanzania katika alama ya dunia kimataifa, kuja kwa marais hawa si jambo dogo na linapaswa kuenziwa,’’ alisema.
Alisema licha ya Tanzania kuwa masikini, lakini ni imara katika ramani ya dunia kutokana na ujio wa viongozi wakubwa, na Watanzania hawapaswi kubeza hata kidogo.
Dk. Bana alisema serikali imefanya kazi ya kutosha katika kuitangaza vyema sera ya diplomasia ya uchumi kimataifa, kwa kuwa Rais Obama hakuja nchini kwa ziara ya kitalii.
“Ziara ya Rais Obama ni ya kikazi, ndiyo maana amefuatana na kundi la watu na wasaidizi wake, hivyo ni wakati muafaka kwetu kuitumia fursa hiyo kwa kuunganisha ushirikiano wa kibiashara,’’ alisema.
Naye Profesa Sifuni Mchome, ambaye ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), alisema ziara ya Rais Obama ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa taifa.
“Tukae na kuangalia ni maeneo yapi tunayopaswa kuwekeza nguvu katika ushirikiano wa kidiplomasia, kwa kuwa bado tuna matatizo katika baadhi ya maeneo, hususan elimu na teknolojia,’’ alisema.
Alisema serikali iendelee kuzitumia kikamilifu ziara za viongozi hao kujenga ushirikiano wa kidiplomasia katika maeneo ambayo bado yapo nyuma na yanahitaji msukumo ili kusonga mbele.
Wednesday, 3 July 2013
JK: Asanteni
09:10
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru