Wednesday 10 July 2013

Stars funga Uganda CHAN


NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) imeitaka timu ya taifa, 'Taifa Stars' kuhakikisha inaifunga Uganda katika mechi yao ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la CHAN.
Changamoto hiyo ilitolewa juzi na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe wakati wa hafla ya chakula cha usiku alichowaandalia wachezaji wa timu hiyo kwenye hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam.

Taifa Stars na Uganda zinatarajiwa kushuka dimbani keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Kampala, Uganda.
Kavishe amewataka Watanzania kutokata tamaa baada ya Taifa Stars kushindwa kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 baada ya kupata kipigo cha mabao 4-2 kutoka kwa Ivory Coast.
Alisema kiwango cha Taifa Stars kwa sasa kipo juu na iwapo wachezaji watacheza kwa ari na kujituma, inao uwezo mkubwa wa kufuzu kucheza fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
"Tumeshindwa kwenda Brazil, basi twende Afrika Kusini mwakani. Sisi kama wadhamini wa Taifa Stars tuna imani kubwa kwamba tutaishinda Uganda katika mechi zote mbili na kufuzu kucheza fainali kwa mara ya pili,"alisema Kavishe.
Meneja huyo wa bia ya Kilimanjaro alisema, TBL imefarijika kuona Taifa Stars imepiga hatua kubwa kimaendeleo tangu walipoanza kuidhamini mwaka jana.
Kavishe pia alitumia fursa hiyo kutoa zawadi maalumu kwa wachezaji wa Taifa Stars, ambazo ni pamoja na DVD zilizorekodiwa maelezo (profiles) ya kila mchezaji, kazi ambayo ilifanywa kitaalamu kwa udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager.
Alisema wachezaji wanaweza kuzitumia DVD hizo kwenye mitandao ili waweze kujitangaza na kujulikana vizuri ndani na nje ya nchi.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen aliwashukuru wadhamini hao na kusema: ìKwa kweli mmekuwa zaidi ya wadhamini maana ushirikiano mliioonyesha ni wa hali ya juu.î
Alisema wachezaji wana ari kubwa sana kwani matunzo wanayopata hivi sasa ni ya hali ya juu na wote wanalenga kupata mafanikio.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru