Sunday, 7 July 2013

Ongezeni thamani ya mazao ya nyuki - Pinda


NA KHADIJA MUSSA
SERIKALI imewataka wawekezaji wa ndani na nje, kuwekeza kwa kuyaongezea thamani mazao ya nyuki nchini.
Imesema kwa kufanya hivyo, kutasaidia kuongeza ajira na kipato kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Pia, imewataka wafanyabiashara na taasisi za kuagiza na kuuza vifaa vya ufugaji na uchakataji wa mazao ya nyuki, kuwawezesha wafugaji kupata vilivyo bora kwa ajili ya uhifadhi na ufugaji wa mazao hayo kwa gharama nafuu.

Hayo yalisemwa jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, katika maadhimisho ya Siku ya Asali, yaliyofanyika katika viwanya vya Maonyesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Pinda, alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na makundi ya nyuki milioni 9.2, yenye uwezo wa kuzalisha asali tani 138,000 na tani 9,200 za nta, kwa mwaka.
Kwa sasa Tanzania inazalisha wastani wa tani 8,153 za asali na wastani wa tani 578.78 za nta kwa mwaka.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda alisema, kiasi cha asilimia 4.5 ya asali ndicho kinachouzwa nchi za nje na kilichobaki kinatumika nchini, huku asilimia 66 ya nta ikiuzwa nje ya nchi.
“Kwa ujumla, kiwango cha asali tunayozalisha kikilinganishwa na fursa zilizopo, inaonyesha kuwa tunatumia asilimia 6.7 ya fursa zilizopo.
“Vivyo hivyo kwa upande wa nta, matumizi ni asilimia 6.5 ya fursa zilizopo,” alisema Pinda.
Alisema sekta ya nyuki ina fursa kubwa za soko la ndani na nje ya nchi.
Takwimu zinaonyesha kuwa tani 400,000 za asali huingia katika soko la dunia, lakini mauzo ya Tanzania ni madogo licha ya asali yake kukubalika katika soko hilo, baada ya Nchi za Umoja wa Ulaya kuridhia.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingine toka barani Afrika zinazouza asali katika soko hilo ni Zambia, Ethiopia, Cameroon na Uganda.
Waziri Mkuu Pinda, pia alizindua Rajamu ya Tanzania (asali yenye ubora wa juu), ambayo imepata soko nchini Marekani na kuwataka wazalishaji wake kuzingatia ubora na kuheshimu mikataba iliyokubaliwa.
Akizungumzia ajira zitokanazo na sekta ya nyuki, Pinda alisema mpaka sasa inatoa ajira takribani milioni mbili.
Alisema ni miongoni mwa sekta zenye fursa wazi ya ajira.
Alisema tayari serikali imeshazielekeza halmashauri zote nchini, kuanzisha kitengo maalum cha nyuki, kwa lengo la kusogeza huduma za ugani karibu na wafugaji.
Pia, alizitaka halmashauri ambazo bado hazijaanzisha vitengo hivyo, kuharakisha kuvianzisha.
Katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu Pinda alipata fursa ya kutoa tuzo mbalimbali kwa washiriki wa maonyesho hayo.
Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), lilifanikiwa kutwaa tuzo za jumla na nafasi ya pili ilichukuliwa na Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji (EPZA), huku ya tatu ikienda  Chuo Kikuu cha Ardhi.
Kwa upande wa Serikali, nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, ya pili Wizara ya Fedha na Wizara ya Nishati na Madini ilishika nafasi ya tatu.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Abdallah Kigoda, alisema wizara inaendelea kutoa elimu kuhusiana na faida zitokanazo na sekta ya nyuki

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru